Serikali kupitia
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA)
imesaini mkataba na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering
Construction Cooperation (CCECC) ya China kwa ajili ya ujenzi wa mradi
wa maji wa Kyaka- Bunazi wenye thamani ya shilingi 9,414,739,257.50.
Akizungumza
hivi karibuni wakati wa kusaini mkataba huo kwenye Ofisi za MWAUWASA,
Jijini Mwanza, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard
Msenyele aliipongeza kampuni hiyo kwa kushinda tenda na alibainisha
kwamba ujenzi wa mradi huo utachukua miezi 13.
Alisema
mkataba unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji kwenye Mto Kagera chenye
uwezo wa kuzalisha lita za maji 6,574,000 kwa siku; ulazaji wa bomba kuu
kutoka kwenye chanzo hadi kwenye kituo cha tiba ya maji; ujenzi wa
kituo cha tiba ya maji kitakachokuwa na tenki la kuhifadhia maji.
Alibainisha
kwamba kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wananchi wa maeneo ya
Kyaka, Bunazi na maeneo mengine yanayozunguka mradi Wilayani Missenyi.
Mhandisi
Msenyele alimsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo kwa
wakati na kwa ubora unaotakiwa kama ilivyo kwenye mkataba. “Ni vyema
Mkandarasi ukatambua suala la muda, hakikisha mradi unakamilika kwa
wakati, wananchi wanausubiri huu mradi kama walivyoahidiwa,” alisisitiza
Mhandisi Msenyele.
Mara baada ya
kusaini mkataba, Mhandisi Msenyele alimtaka Mkandarasi kuelekea eneo la
mradi kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kuanza ujenzi hasa
ikizingatiwa kwamba ujenzi wa mradi ulipaswa kuwa umekwisha anza.
“Hakuna
sababu ya kuchelewa, mipango yote ipo tayari na kwakuwa tumekwisha saini
mkataba ni vyema ukafika eneo la mradi na kujipanga ukiwa huko huko,
suala la muhimu kwa sasa ni nyinyi kufika eneo la mradi,” alisisitiza
Mhandisi Msenyele.
Kwa upande
wake Mhandisi Mradi wa Kampuni ya CCECC, Mhandisi He Jun alimhakikishia
Mhandisi Msenyele kwamba watahakikisha wanakamilisha mradi kwa wakati na
kwa ubora unaotakiwa kama ilivyo kwenye mkataba.
Ujenzi wa
mradi wa maji Kyaka Bunazi ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Julai 11,
2019.
Akiwa njiani
akitokea Wilayani Karagwe kuelekea Wilayani Chato, Rais Magufuli
alisimama katika Mji Mdogo wa Kyaka kusalimiana na wananchi ambao
walimueleza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na
salama.
Kufuatia hali
hiyo, Rais Dkt. Magufuli alimuelekeza Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa kuhakikisha anafika eneo hilo ili kutazama namna ya kuwa na
mradi utakaotumia maji kutoka Mto Kagera.
Waziri
Mbarawa alifika eneo hilo na alielekeza Mamlaka ya Maji Mwanza
(MWAUWASA) kushirikiana na Mamlaka ya Maji Bukoba na Wakala wa Maji
Vijijini kuratibu upatikanaji wa mradi huo.
MWAUWASA
ilipewa jukumu la kusimamia hatua zote za ujenzi wa mradi kwa niaba ya
Wizara ya Maji kuanzia mchakato wa upatikanaji wa Mkandarasi
atakayeutekeleza.
Aidha,
Mhandisi Msenyele alibainisha kwamba japo agizo lilikuwa kuwapelekea
maji wananchi wa eneo la Kyaka lakini baada ya kufanyika kwa tathmini
ilionekana kuwa hata mji wa Bunazi ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya
Missenyi napo palikuwa na uhitaji mkubwa wa maji.
Aliongeza
kuwa kufuatia tathmini hiyo, ilibidi usanifu na utayarishaji wa mradi
uhusishe pia maeneo hayo mengine yaliyokuwa na uhitaji wa maji ili
kujengwe mradi wenye uwezo wa kuhudumia maeneo yote na kwamba suala hilo
limechangia kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa mradi.
0 Comments