TANGAZA NASI

header ads

Naibu waziri Kanyasu akerwa na wavamizi wa maeneo ya hifadhi

 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameonesha kukerwa  na baadhi ya wananchi  wanaendelea kujenga nyumba na kuendesha shughuli za kilimo katika maeneo yenye  Wanyamapori hasa katika mapito ya Wanyamapori katika eneo la Kwakunchinja linalounganisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Manyara.

Amesema kutokana na tabia hiyo  Serikali haiwezi kumaliza kulipa vifuta jasho na vifuta machozi kwa wananchi wanaoshambuliwa na wanyamapori wakali na waharibifu

Ameyasema hayo  wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa  Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (WMA)  iliyopo wilaya ya  Babati mkoani Manyara kuona namna ya kulinda ushoroba wa Kwakunchinja ambao ni umuhimu kwa  Wanyamapori wanaotoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kuelekea Hifadhi ya Ziwa Manyara.

Amesema kwa mwaka huu pekee Serikali imetumia kiasi cha shilingi Bilioni moja kulipa vifuta jasho na vifuta machozi huku kiasi cha shilingi Bilioni 2.3 ikiwa bado hakijalipwa kwa wananchi walioathiriwa na Wanyamapori wakali na Waharibifu

Amesema kila mahali wananchi wamekuwa wakilalamikA kuchelewa kulipwa vifuta jasho na vifuta machozi kutokana na madai hayo kuwa mengi hali inayopelekea Wizara kuwa na madai mengi yasiyolipika  kutoka kwa wananchi ambao baadhi wameyafuata makazi ya Wanyamapori

 Hata hivyo, Mhe.Kanyasu amesema Serikali inatafuta mbinu mbadala ya kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu baada ya kugundua kuwa fidia sio suluhisho kutokana na wimbi kubwa la wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu katika shoroba za wanyamapori pamoja na maeneo ya mitawanyiko ya wanyamapori .

Amesema kutokana na tabia  ya baadhi ya  wananchi kufanya makazi katika maeneo hayo, Wizara ya Maliasili na Utalii imegundua hata ikitenga bajeti nzima ya Wizara kwa ajili ya kulipa vifuta jasho na vifuta machozi haitaweza kumaliza tatizo hilo.

 Mhe.Kanyasu amesema binadamu wamekuwa wakiwafuata Wanyamapori hivyo suala la mazao ya kushambuliwa ni jambo lisiloepukika

""Sehemu ya Mapori ya Akiba na Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori ndimo Wananchi wameanzisha makazi hivi unategemea wanyamapori watulie tu " alihoji Kanyasu.

Amefafanua kuwa Wananchi waliojenga katika maeneo hayo wamekuwa wakitoa visingizio kuwa ardhi imepungua na hivyo kuwalazimu kuanzisha shughuli za binadamu katika maeneo ya wanyamapori suala ambalo ni umekuwa ni mzigo kwa Serikali ya kuanza kulipa fidia kila mwaka.

Amesisitiza kuwa shida sio ardhi bali wananchi wameshindwa kutumia ardhi waliyonayo kimipango hata hivyo Wananchi walio wengi wanataka kufuga mifugo kwa idadi kubwa na sio kwa ubora.

Pia, Akizungumzia Kilimo, Mhe.Kanyasu amesema Wakulima wamekuwa wakilima kizamani kwa kuamini kulima eneo kubwa ndio kupata mazao mengi jambo ambalo si kweli.

Amesema shida kubwa inayoikabili nchi kwa sasa ni ongezeko kubwa la binadamu na mifugo ilhali ardhi haiongezeki.

Amesema hali hivyo imechangia maeneo ya Hifadhi kuvamiwa kwa ajili ya kilimo na makazi kwa vile maeneo hayo yamehifadhiwa na hiyo haimaanishi kuwa hakuna vijiji vyenye maeneo kwa ajili ya makazi na malisho ya mifugo.

" Vijiji vyote vina mabonde, vijiji vyote vina maeneo ya malisho lakini yameharibiwa kutokana na idadi kubwa ya mifugo na mengine yameharibika kwa vile hayatunzwi" alisisitiza Kanyasu

Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu amezitaka taasisi za Uhifadhi nchini kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze  kutambua umuhimu wa maeneo yaliyohifadhiwa la sivyo migogoro kati ya binadamu na wanyamapori haitaisha.

Hata hivyo, Amewataka wananchi kubadili mfumo wa maisha kwa kuacha  kufuga kimazoea badala yake wafuge  kisasa na pia waachane na kilimo cha kuhama hama ambacho kutokana na ongezeko la idadi ya watu hakifai kwa sasa .

Post a Comment

0 Comments