Na Editha Karlo,Kigoma
Wanachama wa Chama cha Waandishi wa habari wa Mkoa wa Kigoma (Kigoma
Press Club - KGPC) wamewachagua viongozi wapya wa chama hicho katika
nafasi mbalimbali ambao wataongoza kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia
mwaka huu 2020 hadi mwaka 2025.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumamosi Mei 16,2020 katika
ukumbi wa ofisi za KGPC Mwenyekiti wa uchaguzi huo Richard Katunka
ambaye ni Mwandishi wa Star tv Mkoani Kigoma alisema Mwenyekiti mpya wa
chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Kigoma ni Deogratius Nsokolo,huku
nafasi ya makamu Mwenyekiti ikichukuliwa na Jacob Ruvilo.
Amesema wanachama wamemchagua Deogratis Nsokolo kwa kura wajumbe wote
28 kumpigia kura za ndiyo kuwa mwenyekiti mpya ambayo ni nafasi yake
aliyokuwa anaitetea.
Nsokolo ambaye ni mwandishi wa ITV Mkoa wa Kigoma pia Rais wa Muungano
wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini Tanzania (UTPC) aligombea nafasi
hiyo ya Mwenyekiti akiwa hana mpinzani hivyo wajumbe walimpigia kura za
ndiyo na hapana na kufanikiwa kunyakua kura zote za ndiyo.
Nafasi ya makamu mwenyekiti imenyakuliwa na Jacob Ruvilo mwakilishi wa
Azam Tv Mkoa wa Kigoma aliyeshinda kwa kura 22 za ndiyo ambapo nafasi
hiyo alikuwa anaiwania peke yake.
Nafasi ya katibu Mkuu wa KGPC ilichukuliwa na Mwajabu Hoza mwakilishi wa
Channel Ten Mkoa wa Kigoma baada ya kupata kura 15 na kumshinda
mpinzani wake Fadhil Abdallah mwandishi wa Magazeti ya TSN aliyekuwa
akitetea nafasi yake aliyepata kura 9 huku Rhoda Ezekiel mwandishi wa
gazeti la Uhuru alijitoa kwenye nafasi ya kugombea ukatibu na nafasi ya
katibu msaidizi ikichukuliwa na Emanuel Senny mtangazaji wa radio Joy
aliyepata kura 22.
Nafasi ya Mweka hazina ilichukuliwa na Winne Bwire kwa kupigiwa kura za ndiyo 27 kati ya kura 28.
Kwa upande wa wajumbe wa kamati tendaji waliochaguliwa ni Prosper
Kwigize mwakilishi wa DW aliyepata kura 14 Happy Tesha mwandishi wa
gazeti la Mwananchi kura 15 na Adrian Eustate mtangazaji wa radio
Kwizera aliyepata kura 23 jumla ya wagombea sita walijitokeza kugombea
nafasi hizo.
Akizungumza baada ya uchaguzi Mwenyekiti mpya Deogratias Nsokolo
aliwapongeza wajumbe kwa kumchagua na kuendelea kuwa na imani naye
kuendelea kuongoza KGPC kama mwenyekiti aliahidi ushirikiano ili
kuendeleza Klabu hiyo na kuwataka wanachama kutoa ushirikiano kwa
uongozi huo mpya.
Aliwataka pia wanahabari kuchukua tahadhari wanapokuwa katika majukumu
yao ya kazi kutokana na janga hili lililopo sasa la virusi vya Corona
"Wakati tulionao sasa ni wakati wa hatari kwa sababu ya ugonjwa huu wa
virusi vya Corona na kazi zetu hizi kuna kipindi inatulazimu
kujitumbukiza kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu tuwe na tahadhari
ugonjwa huu hautahangalia eti wewe ni mwandishi tuchukue tahadhari kama
tunavyoshauriwa na wataalam wa afya juu ya ugonjwa huu",alisema Nsokolo
Pia aliwataka waandishi kutumia kalamu zao kuelimisha jamii namna ya
kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kufuata maelekezo ya
wataalam wa afya.
Naye mwanachama Antony Kayanda amewataka viongozi hao wapya kuendeleza
yale mazuri yote yaliyofanywa na uongozi uliopita ili kuendeleza Klabu
hiyo ambayo imekuwa mfano kwa Klabu zingine nchini.
Naye mwanachama Magreth Magosso Abdallah amewapongeza viongozi wote
waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali na kuwataka kuendeleza yale
mazuri yote yaliyoanza kufanywa na viongozi waliomaliza muda wao.
"Nina wapongeza nyote mlioshinda na kutangazwa na mlioshinda lakini
kura hazikutosha nawapongeza pia tusonge mbele tuijenge KGPC yetu nguvu
yetu inatosha kukipeleka chama chetu mbele",alisema
0 Comments