Na Mwandishi wetu-NCAA
Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imezindua mfumo mpya wa Utalii Mtandao
“Tourism Web Camera” unaolenga kuwaleta pamoja watu mbalimbaali duniani
kuona vivutio vilivyopo katika hifadhi ya Ngorongoro hasa katika kipindi
hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 ambapo wageni wengi wamefungiwa
katika nchi zao.
Uzinduzi wa
Mfumo huo uliohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii
Prof. Adolf Mkenda umelenga kuunganisha watu mbalimbali ulimwenguni
kuweza kufuatilia vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo ambapo kwa
kuanzia watazamaji wataona vivutio hivyo bure na baadae kuchangia kiasi
kidogo cha pesa katika kuendeleza uhifadhi wa rasilimali na vivutio
katika hifadhi hiyo.
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda ameelezea
kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na NCAA katika kuwafikia wadau wake
pamoja na kukabiliana na changamoto za ukosefu wa wageni kutokana na
Janga la Korona.
Amebainisha kuwa
shughuli za ulinzi na uhifadhi wa rasilimali ndani ya hifadhi ni suala
endelevu na lazima kuendelea kuwahabarisha wageni kuhusu yanayojiri
ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro hasa kipindi hiki ambacho wengi
wamezuliwa kusafiri.
“Tunajua kuwa
kwa sasa watalii wengi nchi zao ziko kwenye ‘lockdown’ na hawawezi
kusafiri, NCAA mmefanya kitu chenye maana katika kutafuta namna ya
kuwafikia hukohuko walipo na kuendelea kufurahia utalii wa Ngorongoro
popote duniani, ni imani yangu kuwa hatua hii itasaidia kuwaandaa watu
kisaikolojia wasisahau kuhusu vivutio vya Ngorongoro hata baada ya janga
hili kupita” ameongeza Prof Mkenda.
Prof Mkenda
ameongeza kuwa Mtazamo wa Rais Dkt John Pombe Magufuli ni kuhakikisha
kuwa tunaendelea kujilinda na kujipanga huku tukihakikisha kuwa baada ya
janga la CORONA kupita uchumi wa nchi yetu unarudi kama ulivyokuwa.
Kamishna wa
Uhifadhi wa NCAA Dkt Freddy Manongi amebainisha kuwa mfumo huo wa utalii
mtandao kwa njia ya “Live streaming web camera” uliozinduliwa unalenga
kuwafikia watu mbalimbali duniani kuona bure kwa kufungua Youtube
channel na kuandika neno Ngororongoro Conservation Areakwa ajili ya kufuatilia vivutio katika hifadhi hiyo.
“Tumeshuhudia
anguko katika sekta ya Utalii baada ya janga la Covid 19 ambapo kwa
sasa inapita siku nzima bila kupata mgeni hata mmoja, kwa hiyo tumeamua
kubuni teknolojia hii ya kuwaleta pamoja wateja wetu duniani kote ambao
kupitia mfumo huu wataona vivutio vya Ngorongoro Mubashara wakiwa
majumbani mwao”
Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa NCAA anayesimamia Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano Bw. Jocktan Bikombo amebainisha kuwa mfumo huo wa ‘live
streaming’ umeunganishwa na Camera mbalimbali zilizofungwa ndani ya
hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha kuwa wateja wetu wanapata ladha
tofauti ya vivutio vilivyopo.
Uzinduzi wa
mfumo huo umeenda sambamba na majaribio ya kuunganisha moja kwa moja
wadau mbalimbali waliopo Paris nchini Ufaransa na London Nchini
Uingereza ambao wamethitbitisha kuuona na kushuhudia vivutio hivyo kwa
njia ya mtandao.
0 Comments