HALMASHAURI
ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha imetumia zaidi ya shilingi milioni 308
kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika kipindi Cha mwaka wa
fedha 2019//2020 hadi kufikia Aprili 15 mwaka huu.
Akizungumza
leo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru Emmanuel Mkongo amesema
kuwa halmashauri hiyo katika kuunga mkono jitihada za wananchi
kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020
ilitenga kutoka katika makusanyo ya mapato ya ndani jumla ya shilingi
milioni 515.
Na kutumia shilingi milioni 308 katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ujenzi
kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba 21 vya madarasa na vyumba 3
vya maabara sambamba na ununuzi wa viti na meza
Amesema kuwa
ikiwa ni mkakati wa Halmashauri hiyo kuendelea kuboresha miundombinu ya
sekta ya elimu kwa kukamilisha vyumba vya madarasa na maabara ili
kutatua changamoto ya msongamano wa wanafunzi kutokana na ufaulu mkubwa
wa wanafunzi walioingia kidato cha kwanza mwaka huu na mkakati wa
kuboresha ufundishaji wa masomo ya Sayansi.
Aidha , akizungumza
wakati wa kukabidhi vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh. 18,961,020.06
kwa Shule ya Sekondari Maroroni na Sing'isi kwa ajili ya ujenzi wa
vyumba vya madarasa na maabara, Mkongo amesema vifaa hivyo vimegawanywa
kwenye Kata zote 26 kwa kutoa kipaumbele kwa Kata ambazo Wananchi wake
wameonesha juhudi za kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo akitolea
mfano Kata ya Maroroni na Sing'isi na kutoa wito kwa wananchi wa Kata
nyingine kufanya vizuri zaidi.
Ameongeza kuwa fedha hizo
jumla ya Shilingi milioni 308 za mapato ya ndani ya Halmashauri na
Shilingi 50,666,300 za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo ambao
Mwenyekiti wa Kamati ya ya Mfuko huo ni Mbunge wa Jimbo la Arumeru
Mashariki Dkt. Danielson Pallangyo zimechochea kwa kiasi kikubwa ujenzi
na ukamilishaji wa Miundombinu hiyo.
Aidha, Mtendaji wa Kata ya
Maroroni Lyidia Sarakikya amemshukuru Mbunge Dkt.Pallangyo na
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru kwa kutoa mbao, bati na
mifuko ya saruji kwaajili ya kukamilisha vyumba 3 vya madarasa kwani
imewatia wananchi moyo kwa kupunguza ukali wa michango.
Wakati
huo Mkuu wa Shule ya sekondari Maroroni Mwalimu Felix Nibigira
aliishukuru Serikali na kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi
kutokubweteka kipindi ambacho shule zimefungwa badala yake wawasimamie
wanafunzi kufanya mazoezi yaliyotolewa kwani shule hiyo iliwaandalia
majaribio na masomo kwa kifurushi kilichopewa jina la HOME PACKAGE.
0 Comments