NA FREDY MGUNDA, IRINGA.
Kaimu Meya wa Manispaa ya Iringa Joseph Nzala Ryata amezindua rasmi mkakati maalum wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wa Ukarabati wa barabara za kata 18 zilizoharibika kutokana na mvua zzilizonyesha katika msimu wa masika.
Wakati wa Uzinduzi wa Mkakati huo wenye lengo la kuondosha changamoto ya baadhi ya maeneo kutofikika kirahisi na kukwamisha maendeleo ya wananchi wa manispaa ya Iringa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo kaimu meya alisema kuwa halmashauri imekuja na mkakati wa kuhakikisha wanakarabati barabara zote zilizoharibiwa na mvua ya msimu huu na kurahisisha shughuli za wananchi kuendelea kama ilivyokuwa hapo awali.
Alisema mvua za msimu huu zimeharibu barabara pamoja na kuvunja madaraja madogo na makubwa na kusababisha kukatika kwa mawasiliano katika baadhi ya mitaa ya kata za manispaa hiyo na kusababisha shughuli za kiuchumi kuzorota.
Ryata alisema sababu ya kuanza kukarabati barabara ya mtaa wa Kihondombi ni kutokana na umuhimu wa barabara hiyo ambayo hutumika kama mbadala wa barabara kuu iendayo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo mkoani Iringa.
“Ikitokea ajali yoyote itakayolazimisha kufungwa kwa barabara kuu iendayo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na endapo barabara ya Kihodombi haipitiki ni wazi kuwa ni ngumu kwa watalii na watu mbalimbali kufika katika maeneo wanayotakiwa kufika kwa mjibu wa watuaji wa barabara hiyo,hivyo ni sasabu mkuu ya kuanza ukarabati wa barabara hii kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla” alisema Ryata
Aidha Ryata alisema kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi juu ya ubovu wa barabara ambazo zilikuwa zinasababisha usumbufu wa usafiri katika meneo mengi ya mitaa ya manispaa ya Iringa ambazo zilikuwa zinasababisha kushuka kwa uchumi wa wananchi.
Kwa upande wa baadhi ya wananchi wa maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Iringa wamepongeza mpango huo wa Manispaa wakieleza kwa muda sasa shughuli mbalimbali za kiuchumi zimekuwa zikikabiliana na changamoto kuu ya miundombinu duni ya barabara kutokana na vyombo vya usafiri kushindwa kufika kwa wakati katika maeneo husika huku wakilazikia kutumia gharama kubwa zaidi.
Nao viongozi wa Serikali za mitaa ya kata ya Kihodombi Manispaa ya Iringa wameeleza kuwa hatua hiyo inayosimamiwa na Kaimu Meya wa Manispaa ya Iringa ni ya kipeekee kwani hakuna mwananchi anayechangishwa fedha ili kukarabati barabara hizo zilizosahalika kwa muda mrefu na kusababisha wananchi kuichukia Serikali yao
0 Comments