Na Clief Mlelwa,Njombe
Walimu nchini wametakiwa kuutumia ipasavyo muda
ambao umetengwa kwaajili ya michezo katika kuibua vipawa vya wanafunzi ili
kuwajengea uwezo wa kujiajiri pindi wanapohitimu masomo yao kwa ngazi tofauti.
Wito huo umetolewa na mgeni rasmi Padre wa jimbo
la Njombe INNOCENT CHAULA katika hafla ya tamasha la kubaini vipawa vya
wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Collegine iliyopo kijiji cha
Ilunda wilaya ya Njombe,ambapo amesema kuwa masomo ya darasani pekee hayatoshi
kuwajengea uwezo wa kujiajiri wanafunzi.
Aidha Padre Chaula amesema kuwa endapo muda
ambao umetengwa kwaajili ya michezo ukatumiwa ipasavyo hasa katika kuibua
vipawa vya wanafunzi,kuwashirikisha katika shughuli za ulimaji wa bustani za
shule itawasaidia zaidi wanafunzi hao kujitambua na kujua namna sahihi ya
kuishi pindi wanapohitimu elimu yao.
“Mwanafunzi halelewi tu kwa kusoma vitabu,lazima
ajifunze namna ya kusoma,kujitegemea lakini pia ni katika burudani na michezo
ni vema mwanafunzi awe na zile stadi anazoweza kuishi nazo hata katika
jamii”alisema Padre Chaula
Wakizungumzia kuhusiana na tamasha la kubaini
vipawa vya wanafunzi wa shule hiyo ya collegine mwalimu wa shule hiyo FRANCE
KIHOMBO na sister NOELA FEDRICK wamesema kuwa kupitia tamasha hilo wamebaini
vipawa mbalimbali vya wanafunzi wao ikiwemo kuimba na kuigiza.
“Michezo inamjengea motto hali ya
kujiamini,kujenga kipaji chake kitu ambacho hapo baadaye kinaweza kuja kumletea
manufaa kutokana na vipaji vile walivyo navyo”alisema mwalimu Kihombo
Hata hivyo wanafunzi wa shule hiyo wamesema kuwa
kufanyika kwa tamasha hilo kunawapa elimu sahihi ya namna ya kuishi mara baada
ya masomo yao na kujiepusha na vitendo vya kujihusisha na mahusiano ya
kimapendi pindi wakiwa shule.
“Manufaa ni kukuza vipaji vyetu lakini pia
kupunguza mawazo yale tunayoweza kuwa nayo kwasababu michezo inatujenga kimwili
na kiakili”walisema wanafunzi
Tamasha hilo limehusisha michezo mbalimbali
ikiwemo,kukimbia umbali wa kilomita tatu,kukimbiza kuku ,kuimba,kuigiza na
kucheza mpira wa mikono na miguu.
0 Comments