TANGAZA NASI

header ads

Wakulima wa chai watakiwa kuboresha teknolojia ya uchumaji majani

 


Na Amiri Kilagalila,Njombe

Wakulima wa chai nchini wametakiwa kuboresha teknolojia ya uchumaji chai kutoka kuchuma kwa mikono hadi kwa mashine na kupata chai iliyobora  ili kuendana na mahitaji ya soko la Dunia.

Hayo yalisemwa  na meneja mkuu wa kiwanda cha chai Kibena Mohamed Kasila baada ya kutembelewa na wadau wa chai kutoka mikoa mitano ya hapa nchini walioshiriki mafunzo kwa vitendo katika kiwanda hicho kilichopo mkoani Njombe yaliyoandaliwa na mradi wa Mark Up unaofadhiliwa na umoja wa ulaya. 

Amesema duniani kwasasa sekta ya chai imekumbwa na changamoto ya kuanguka kwa bei kwenye soko la dunia hivyo njia pekee ya kuinasua sekta hiyo ya chai ni kuhakikisha wanazalisha chai yenye ubora kwa kufuata kanuni bora za kilimo, kanuni bora za uchakataji ili iweze kufika sokoni ikiwa na ubora wa hali ya juu.

Amesema kupitia mafunzo waliyoyapata mameneja wa mashamba, wakaguzi wa mashamba ya chai na waliopo katika uchakataji utasaidia kupata chai yenye viwango itakayouzwa kwa bei nzuri sokoni na kushindana na makampuni mengine kutoka sehemu mbalimbali duniani yanayozalisha chai.

Ameiomba Markup kusaidia mchakato wa kupata masoko nje ya nchi wakati serikali ikiwa kwenye mchakato wa kuanzisha mnada wa chai hapa nchini.

"Katika huo.mnada ili tufanye vizuri ubora wa chai inayozalishwa hapa nchini ni kitu cha msingi tusipokuwa na chai bora mnada huo tutakaofungua hautofanya vizuri" amesema Kasila.

Mratibu wa mradi wa Markup Tanzania unaojishughulisha kusaidia wazalishaji na wajasiriamali kuongeza thamani ya mazao yao na kupata masoko Safari Fungo alisema  kwa muda wa siku mbili wamekuwa na mafunzo ya nadharia kwa wajasiriamali na wazalishaji ili kuwajengea uwezo na siku mbili nyingine watakuwa kwenye mafunzo ya vitendo kwa kufika kwenye mashamba ya chai na kuangalia vitu vya kuzingatia katika kuzalisha chai iliyo bora.

"Uzuri wake ni kwamba wanapata nafasi ya kuweza kushirikiana na kupeana uzoefu na wazalishaji wengine kwasababu tuna wazalishaji wengi kutoka viwanda mbalimbali hapa nchini " alisema  Safari.

Alisema  siku ya mwisho ya mafunzo hayo wataingia katika sehemu ya masoko hii ni baada ya kujifunza namna ya kuongeza thamani ya zao hilo la chai.
 
"Wamepata kile ambacho soko linahitaji sasa ni namna gani ya kupata masoko mazuri duniani pamoja na ukanda huu wa jumuiya ya  Afrika mashariki hiyo hasa ndiyo dhamira yetu" alisema  Safari.

Aliushukuru umoja wa nchi za ulaya kwa kuwa sehemu ya kutoa ufadhili katika mradi wa Markup pamoja na Kibena tea ambao wamekubali kiwanda chao kuwa sehemu  ya kuweza kuendesha mafunzo hayo kwa njia ya vitendo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo meneja uzalishaji Stanslaus Benela na meneja mashamba kutoka kiwanda cha chai Kibena walisema  mafunzo hayo yatawajengea ujuzi kwa kuongeza ubora kwa kile wanachokizalisha shambani nakupunguza gharama za uendeshaji ili wawekezaji wapate faida zaidi.

 "Kupitia Markup na program hii waliyoifanya sisi tumeifurahia sana kwani imetuongezea ujuzi zaidi na kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji" alisema  Stanslaus.

Post a Comment

0 Comments