TANGAZA NASI

header ads

MAHAKAMA YA KISUTU YAUTAKA UPANDE WA MASHTAKA KUSHUGHULIKIA MASHAURI YA WATUHUMIWA WANAOTAKA KUKIRI MASHITAKA YAO KWA DPP

  


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewataka Upande wa mashtaka kushughulikia mashauri ya watuhumiwa wanaotaka kukiri mashtaka yao na kuomba kufanya makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kwa hekima na kuzingatia haki za binadamu.


Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi ameyasema hao leo Aprili 22, 2021 wakati kesi ya uhujumu uchumi dhidi ya wafanyabiashara James Rugemalira, Herbinder Seth na Joseph Makandege, kuitwa mahakamani hapo kwa ajali ya kutajwa na wakili wa serikali Mwandamizi,  Wankyo Simon kudai kuwa majadiliano bado yanaendelea

"Sisi wote ni watumishi wa umma  leo upo kwenye nafasi hii lakini muda utafika hautakuwepo tena hapo, hivyo kila mtu anapaswa kushughulikia kwa mujibu wa sheria na taratibu". Amesema hakimu Shaidi.

Amesema, sheria inampa mamlaka DPP ya kukubali ama kukataa maombi ya kukiri makosa yanayowasilishwa kwake na washtakiwa lakini kanuni hazionyeshi baada ya siku 30 za kuingia kwenye majadiliano kuisha nini kitafuata.

Hata hivyo, Washtakiwa walioomba kuingia kwenye majadiliano (bargain) ni Seth na Makandege huku Rugemalira yeye akiomba upelelezi ukamilike.

Mapema jopo la mawakili wanne wakiongozwa Wakili, Alex Balomi, Joseph Sungwa Dorah Mallaba, Kung'e Wabeya na John Chuma kila mmoja aliwasilisha hoja juu ya upelelezi unavyochukua muda mrefu kukamilika,  majadiliano kutokamilika na kuiomba mahakama kuwafutia washtakiwa hao mashtaka na kuwaachia huru.

 Wakili Dorah anayemuwakilisha mshtakiwa Seth amedai siku 30 walizopewa na mahakama kwa ajili ya kumaliza kesi kwa njia ya majadiliano zimepita lakini mpaka leo hawajapata majibu.

Mheshimiwa, hata siku 15 za nyongeza  zimeisha lakini hatujapata majibu yotote, kama DPP anakubali majadiliano asema na kama anakataa basi kesi ifikie mwisho, ushahidi ufungwe kwani upelelezi unachukua muda mrefu bila kukamilika, tunaomba siku 14 kama DPP atakuwa hana majibu ya majadiliano basi kesi ifungwe ama mahakama itumie mamlaka yake kuiondoa kesi hii" amedai Dorah.
 Kwa upande wake wakili wa Rugemalira, John Chuma ameiomba mahakama hiyo iwafutie washtakiwa wote mashtaka yao na kuwaachia huru kwani ni miaka mtano sasa kila siki wanaambiwa upelelezi bado haujakamilika.

Naye, wakili Wabeya anayemuwakilisha mshtakiwa Makandege amedai,  mteja wake na Seth wameonesha nia ya kukaa mezani na DPP ili kumaliza shauri hilo tangia Februari 22, 2021 lakini mpaka leo hawajapata majibu yoyote zaidi ya kuambiwa majadiliano bado yanaendelea.

Amedai kama upande wa mashtaka hawako tayari kuingia kwenye makubaliano ni vema wakaweka wazi ili wajue kama kesi inaendelea ama la.

Akijibu hoja hizo, Wankyo ameiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwani Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwani haijapewa kibali cha kufanya hivyo na pia hoja za utetezi walizowasilisha ni hoja kengefu na hazina mashiko na wala hazina msingi.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakàbiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo kuisababisha Serikali hasara ya dola za Marekani  22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Seth na Rugemarila wanakabiliwa na mashitaka 12 ya uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha Serikali hasara ya dola za Marekani  22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Post a Comment

0 Comments