Na Brigither Nyoni,Makambako
Wananchi mjini Makambako wameiomba serikali kutoa ufafanuzi kuhusiana na mabadiliko ya utoaji wa huduma za afya katika
kituo cha afya Makambako mkoani Njombe baada ya watoto chini ya miaka mitano kutakiwa kulipia
fedha shilingi 4000 ili waweze kumuona daktari na kupatiwa matibabu.
Wakizungumza na mwandishi wetu baadhi ya wanawake
mjini Makambako wamesema kuwa awali
watoto wenye umri chini ya miaka mitano walikuwa wanatibiwa bure lakini kwa
sasa wanaambiwa walipe elfu nne ili wapatiwe huduma.
Akizungumza kwa niaba ya mganga mkuu wa Halmashauri
ya Mji wa Makambako, FROLA MDUGO amekiri kutokea kwa mabadiliko hayo na kueleza
kuwa kwa sasa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanatakiwa kulipia elfu
nne ambayo ni Kwa ajili ya kumuona daktari
lakini upande wa vipimo na dawa watapatiwa bure.
Hata hivyo amesema kuwa kwa wanawake wajawazito kwa
sasa watapatiwa matibabu bure endapo watakuwa na tatizo la afya linalohusiana
na ujauzito lakini kama watakuwa na tatizo la kiafya ambalo halihusiani na
ujauzito wanatakiwa kulipia matibabu yote.
Sera ya Afya nchini Tanzania inataka huduma za Afya kwa wazee, wajawazito
na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupata bure, lakini kumekuwepo na
malalamiko kutoka kwa baadhi ya makundi hayo
kutokana na kutozwa fedha za matibabu.
0 Comments