Mshambuliaji wa Simba anayekipiga kwa mkopo KMC, Charles Ilanfya, amesema kuwa ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri na kumshawishi kocha wa Simba, Didier Gomes amrudishe tena ndani ya kikosi hicho.
Ilanfya alipelekwa KMC kwa mkopo wa miezi sita enzi ya utawala wa aliyekuwa kocha wa Simba Mbelgiji, Sven Vandenbroeck katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15.
Hii ni baada ya kuwa na wakati mgumu kupata nafasi ndani ya kikosi cha Simba mbele ya mastraika Chris Mugalu, Meddie Kagere na John Bocco.
Akiwa na kikosi cha Simba, Ilanfya aliichezea timu hiyo mchezo mmoja tu dhidi ya Tanzania Prisons uliopigwa Oktoba 22, 2020 ambapo Simba walifungwa bao 1-0.
Ilanfya amesema: “Niliondoka Simba ikiwa chini ya kocha Sven Vandenbroeck kwa malengo ya kuja KMC na kupata nafasi zaidi ya kucheza na kupandisha kiwango changu.
“Mambo mengi yamebadilika kwa sasa, Simba imepata kocha mpya na wanaonekana kuimarika zaidi, kwangu kama mchezaji hii inanipa hamasa ya kuendelea kupambana, ili kuhakikisha nakuza kiwango changu na kuweza kupata nafasi ya kurejea tena Simba.”
0 Comments