KUFUATIA mvua kubwa zilizonyeesha na kuharibu makazi ya wananchi wa Kata ya Nkuhungu jijini Dodoma, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kushirikiana na Taasisi ya Msalama Mwekundu Nchini wamegawa misaada kwa wananchi hao.
Mavunde kwa kushirikiana na Taasisi hiyo wamegawa misaada hiyo yenye thamani ya Sh Milioni 35 lengo likiwa ni kuwapunguzia makali wananchi hao waliopoteza makazi pamoja na vifaa muhimu katika kuendesha maisha yao ya kila siku.
Akizungumza katika ugawaji wa msaada huo, Mbunge Mavunde ameipongeza Taasisi ya Msalaba Mwekundu kwa uharaka wake wa kuitikia maombi ya msaada wa vifaa na kuwashika mkono wananchi jambo ambalo limewapa faraja wananchi hao wa Nkuhungu ambao wamekumbwa na mafuriko makubwa ya mvua.
" Niwashukuru sana ndugu zetu wa Red Cross kwa kutufuta machozi katika kipindi hiki, kiasi cha msaada mlichotoa ambacho kinafika Sh Milioni 35 ni kikubwa sana na hakika Mwenyezi Mungu atawalipa, lakini pia nilishukuru Kanisa Katoliki Parokia ya Nkuhungu kwa msaada wa unga, sabuni, mafuta mahitaji ambao yamegharimu Sh Milioni 2.5 hakika mmetugusa sana," Amesema Mavunde.
Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Msalaba Mwekundu Tanzania, David Mwakiposa ametoa pole kwa wananchi kwa tatizo hilo kubwa la mafuriko na kusisitiza kwamba malengo makuu ya Taasisi hiyo ni kusaidia wahitaji pindi wanapopatwa na matatizo na kuwa sehemu ya faraja huku akitoa wito kwa wananchi hao kujiunga na taasisi hiyo ili kuwa sehemu ya faraja kwa wananchi wanaopatwa na majanga mbalimbali.
0 Comments