Na
Amiri Kilagalila,Njombe
Waziri
mkuu, Kassim Majaliwa ameipa siku tatu kuanzia jana Jumatano, Machi 10, 2021
kampuni ya DL iwasilishe maelezo ya kwanini hajawalipa wakulima wa chai fedha
zao tangu mwaka jana hali inayosababisha washindwe kuhudumia mashamba yao.
Ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Machi 10, 2021) wakati akihitimisha kikao na
wadau wa zao la chai kilichofanyika katika ukumbi wa Johnson, mjini Njombe.
Uzalishaji wa chai kavu umeshuka kutoka tani 37,192 kwa mwaka 2018/2019 hadi
tani 28,715 kwa mwaka 2019/2020 kutokana na sababu mbalimbali.
Licha ya kutoa agizo hilo, Pia Waziri Mkuu ameitaka Bodi ya Chai Tanzania
ihakikishe inasimamia ipasavyo zao hilo ili wakulima waweze kunufaika.
“Bodi wajibikeni kwa kusimamia ipasavyo bei ya chai na wawezesheni wakulima
waelewe mfumo unaotumika katika kuuza zao hilo.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa
wawakilishi wa wakulima ambao walidai kuwepo kwa tofauti ya bei ya chai. “Suala
la bei lizingatiwe, mifumo inayotumika katika kuuza chai ieleweke kwa
wakulima.”
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa pembejeo, Waziri Mkuu amesema Serikali
itahakikisha pembejeo zinapatikana ili kumuwezesha mkulima kufanya kazi yake
kwa urahisi na ufanisi zaidi. Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa
pembejeo nchini.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe inatengeneza utaratibu
wa kukutana na wadau ili kujua kero na changamoto zinazowakabili na
kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi.
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie uanzishwaji wa vyama vikuu vya
ushirika wa wakulima wa chai katika maeneo yanayolima zao hilo na vihakikishe
vinakuwa na viongozi wenye nia ya dhati ya kuuendeleza ushirika huo na kuongeza
tija kwa wakulima.
Kadhalika Waziri Mkuu ameiagiza Bodi ya Chai Tanzania (TBT) na Taasisi ya
Utafiti wa zao la Chai (TRIT) zihakikishe zinawafikishia wakulima miche bora na
viuatilifu vinavyotakiwa kwa wakati ili waweze kuiongezea ubora chai inayolimwa
nchini.
Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote zinazolima zao la chai zianzishe
vitalu vya kuotesha miche katika eneo la kuanzia ekari tatu na kuigawa bure kwa
wakulima, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo na
kuongeza uzalishaji.
Akizungumza kuhusu namna ya kuwawezesha Maafisa Ugani kutekeleza majukumu yao
ipasavyo, Waziri Mkuu ameziagiza halmashauri zote zihakikishe zinawapatia
usafiri wa pikipiki ili waweze kuwafikia wakulima kwa urahisi.
Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alisema wizara itayafanyia kazi maagizo
yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu pamoja na maoni ya wadau ili kuhakikisha zao
hilo linaboreshwa. Kuhusu changamoto ya miundombinu ya barabara ziendazo katika
mashamba ya chai ameahidi kuzungumza na TARURA ili kuhakikisha zinapewa
kipaumbele.
Awali Mbunge
wa jimbo la Lupembe Edwin Enos Swale aliiomba serikali kushughulikia sakata la
malipo ya chai kwa wakulima wa Lupembe ambao wamesitisha zoezi la uchumaji wa
majani ya chai tangu march 1 mwaka huu.
0 Comments