TANGAZA NASI

header ads

Mvulani mwenye umri wa miaka 13 aliyehukumiwa kwa kukufuru ashinda kesi

 


Mvulana mwenye umri wa miaka 13 ambaye alipewa hukumu ya kifungo cha muongo mzima cha gerezani kwa kosa la kukufuru mwaka jana sasa atakuwa huru.

Alipatikana na hatia katika mahakama ya kiislamu mwezi Agosti kwa kutoa kauli za kumkufuru Mungu wakati wa mazungumzo na rafiki yake kaskazini mwa Kano.

Lakini mahakama ya rufaa ya serikali ilibatilisha hukumu hiyo Alhamisi, na kusema mshitakiwa alikuwa mtoto.

Hukumu hiyo iliyotolewa mwaka jana mahakama ya sharia ililaaniwa vikali kimataifa.

Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa , Unicef, lilisema ina "ikiuka haki za kimsingi za watoto na haki ya kisheria ya watoto ya Nigeria -na ambayo , jimbo la Kano limeisaini".

Mwezi Septemba wahudumu wa kujitolea 120 , wakiongozwa na mkurugenzi wa makumbusho ya Auschwitz ya Poland , walijitolea kutumikia sehemu ya hukumu ya miaka 10 iliyotolewa awali kwa mvulana huyo.

Maafisa katika jimbo la Kano wanaonekana kutofurahishwa na kutupiliawa mbali kwa kesi dhidi ya mtoto huyo. Mwanasheria mkuu wa jimbo hilo, Musa Lawan ameiambia BBC kuwa watangalia uwezekano wa kukata rufaa.

Kano ni mojawapo ya majimbo 12 yanayotekeleza mfumo wa sheria za kiislamu-Sharia.

Eneo la kaskazini mwa Nigeria linakaliwa na Waislamu wengi , ambako Waislamu hufuata Sharia.

Mahakama ya rufaa pia iliagiza kuanzishwa upya kwa kesi nyingine ya kukufuru, inayomuhusisha muimbaji ambaye alihukumiwa kifo na mahakama ya sharia kwa kutumia maneno katika wimbo wake yaliyoonekana kama ya kumkufuru Mtume Muhammad.

Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Kano aliisifu hukumu hiyo akiitaja kuwa "ushindi kwa watu wa Kano".

Kwa mujibu wa wakili aliye wakakilisha washitakiwa hao wote wawili , "maisha yao hayatarejea kuwa ya kawaida tena ".

Kola Alapinni amesema kuwa haitakuwa salama kwa mvulana huyo kuendelea kuishi Kano , huku muimbaji Yahaya Sharif-Aminu, 22, huenda akaendelea kubaki mahabusu hadi kesi yake itakapoanzishwa tena.

Waandamanaji katika jimbo la Kano waliharibu nyumba ya Bw Sharif-Aminu mwaka jana , na kuilazimisha familia yake kutoroka, liliripoti shirika la habari la Reuters.

Wazazi wa mvulana walijitenga naye kutokana na aibu iliyotokana na kesi , kwa mujibu wa Bw Alapinni.

Kuachiliwa huru kwa mvulana huyo kumekuja kama ahueni kwa watetezi wa haki za binadamu . Lakini jimbo la Kano, ambako wakazi wengi ni Waslamu, kuna uungaji mkono mkubwa wa sharia na na mazungumzo kuhusu kesi ya mvulana huyo ni mdogo.

Badala yake, watu wanazungumzia kuhusu kesi ya Yahaya Sharif-Aminu . Hukumu ya hivi karibuni huenda isiwafurahishe baadhi ya wakazi ambao wamekuwa wakitoa wito auawe, huku wengine watakua wakifuatilia kwa makini kuanzishwa upya kwa kesi kama itaanza.

Kote nchini, hukumu za hivi karibuni zimeibua hisia mchanganyiko na kwa mara nyingine tena kuibua utata usioisha kuhusu utekelezwaji wa Sharia katika baadhi ya majimbo ya Nigeria.

Kano ni miongoni mwa majimbo kumi na mawili ya kaskazini mwa Nigeria yanayotekeleza mfumo wa kisheria wa Sharia sambamba na sheria za kidunia za Nigeria.

Ni Waislamu tu wanaoweza kushitakiwa katika Mahakama za Sharia.

Post a Comment

0 Comments