Na Amiri
Kilagalila,Njombe
Uhaba wa maji safi na
miundo mbinu ya maji taka iliyokuwa kikwazo kwa wajawazito na watoto katika
hospitali ya halmashauri ya mji Njombe (Kibena) imepatiwa ufumbuzi baada ya
kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa tenki la maji katika hospitali hiyo
uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 164.
Hayo yalisemwa juzi na
katibu tawala wa mkoa wa Njombe Catalina Revocat kwenye makabidhiano ya mradi
huo wa tenki la maji lililojengwa katika hospitali hiyo hafla iliyofanyika
katika viwanja vya hospitali hapa mkoani Njombe.
Catalina alisema
upatikanaji wa maji safi katika hospitali hiyo ya halmashauri ya mji awali
ulikuwa duni kiasi cha kutishia afya ya wajawazito na watoto hospitalini
hapo.
Alisema suala la usafi
na afya katika hospitali kwa ujumla inategemea uwepo wa maji safi na utunzaji
wa maji taka ambayo kama hayajashughulikiwa vizuri afya za wagonjwa zinakuwa
hatarini.
Alipongeza shirika la
kuhudumia watoto duniani (UNICEF) na shirika la maendeleo ya watu(PDF) kwa
ujenzi wa tenki hilo la maji kwani kufanya hivyo wameisaidia serikali katika
kuhakikisha huduma za hospitali kwa mama wajawazito na watoto zinakuwa nzuri.
"Hospitali hii
ilijengwa muda mrefu tangu mwaka 1952 wakati huo ilikuwa ikihudumia wagonjwa
wachache lakini mji umekuwa na watu wameongezeka hivyo ilikuwa imezidiwa"
Alisema Catalina.
"Serikali
imejitahidi kujenga miundo mbinu mingi lakini suala la maji na maji taka
mmekuja kutusaidia kuongeza nguvu katika juhudi zinazofanyika na serikali"
Alisema Catalina.
Awali akisoma ripoti
ya utekelezaji wa mradi huo mhandisi wa mradi kutoka PDF mhandisi Elias
Muchunguzi alisema mradi huo ulianza mwaka jana mwezi januari na kukamilika
mwaka huu ambapo mradi huo umelenga kunufaisha watu wapatao 532.
Alisema kwa upande wa
wodi za wazazi ambayo ndiyo kipaumbele cha mradi huo utawanufaisha wajawazito
85 kwa siku katika wodi tatu za wazazi zilizopo kwenye hospitali hiyo.
Aliongeza kuwa
wanufaika wengine wa mradi huo ni wagonjwa waliopo katika wodi zingine ambazo
si za wazazi pamoja na wafanyakazi wa hospitali hiyo ambao ni zaidi ya 187.
" Jumla ya
gharama ya mradi ni shilingi 160, 916,212 hiyo ni kwa upande wa mfadhili lakini
kwa halmashauri imechangia kiasi cha shilingi milioni nne na kufanya mradi huo
kukamilika kwa zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 164" Alisema
Muchunguzi.
Pamela Shao ni mkuu wa
ofisi ya UNICEF nyanda ya juu kusini ambao ni wafadhili wa mradi huo alisema
anaamini maboresho hay ohayo kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto yametatuliwa
kwa kuwa huwezi kutoa huduma ya afya bila maji safi na salama.
“Nadhani kwa mradi huu
ile adha ya zamani kuhusu maji hasa ukifika wodini sasa hivi imeshatatuliwa na
tunajua katika kutoa huduma za afya huwezi kutoa bila ya kuwa na maji safi na
salama”alisema Pamela Shao
Naye mganga mkuu wa
halmashauri ya mji wa Njombe Dkt,Issaya Mwasubila kwa niaba ya mkurugenzi wa
halmashauri ya mji aliahidi kulinda na kuitunza miundombinu hiyo ili iendelee
kuwasaidia watumishi na wagonjwa hususani watoto na akina mama.
0 Comments