TANGAZA NASI

header ads

CCM mwendo wa Mapinduzi tu,Vigogo wang'olewa uenyeviti wa halmashauri,sura mpya zang’aa

 



Na Amiri Kilagalila,Njombe

Wimbi kubwa la mabadiriko ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi limeendelea kwa kasi ambapo hatua ya sasa katika chama hicho ni utaratibu wa kuwachagua wenyeviti wa halmashauri pamoja na Meya watakaokwenda kuwakilisha Chama hicho katika halmashauri zao.

Chama cha Mapinduzi mkoa wa Njombe katika halmashauri zake kimeendelea na uchaguzi wa kuwapata wenyeviti hao huku kwa kiasi kikubwa sura mpya katika nafasi hizo zikionekana kwa kiasi kikubwa katika nafasi hizo.

Katika halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo ameibuka na ushindi Bi Agnetha Mbangile diwani mteule wa kata ya Ulembwe aliyemuangusha mwenyekiti wa muda mrefu Antony Mahwata huku nafasi ya makamu mwenyekiti akishinda Onesmo Lulandala diwani mteule wa kata ya Imalinyi.

Halmashauri zingine ni Njombe mjini aliyeshinda akiwa Starmius Mayemba diwani mteule wa kata ya Njombe mjini huku aliyekuwa mwenyekiti wa muda mrefu Edwirn Mwanzinga jina lake likishindwa kurudi kutoka kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi.Makete aliyeshinda ni Ndg,Francis Chaula diwani mteule kata ya Iwawa huku aliyekuwa Mwenyekiti wake Egnatio Mtawa akiwa nje ya mchakato huo kutokana na awali kugombea nafasi ya Ubunge.

Aidha halmashauri ya wilaya ya Njombe Valentino Hongoli diwani mteule wa kata ya Ikuna akiwa ametea nafasi yake nakufanikiwa kurudi kwa awamu nyingine sawa na halmashauri ya mji wa Makambako diwani mteule wa kata ya Maguvani Hanana Mfikwa akichaguliwa kuwa mwenyekiti na kutetea nafasi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo

Mwandishi wetu ameweka kambi wilayani Ludewa kushuhudia mchakato wa uchaguzi ambapo katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Bakari Mfaume amemtangaza Diwani mteule wa Kata ya Mundindi Ndg, Wise Mgina kuwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Madiwani kwa kupata kura 19 kati ya 32 zilizopigwa na madiwani hao huku mshindani wake, Edward Haule mwenyekiti wa mstaafu akipata kura 13.

Mfaume amesema nafasi hiyo iligombewa na madiwani hao wateule wawili ambapo katika nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na diwani mteule wa Kata ya Mawengi, Leodgar Mpambalyoto ambaye alikuwa mgombea pekee na amepigiwa kura za ndiyo 18 na hapana 14.

Ameongeza kuwa, katika nafasi ya katibu wa kamati hiyo iligombewa na madiwani wawili Diwani wa Masasi, Daudi Mhagama ambaye amepata kura 18 na diwani mteule wa kata ya Lifuma, Michael Haule ambaye amepata kura 14 na kupelekea Daudi kuwa katibu wa kamati ya madiwani na Michael kuwa naibu katibu wake.

Aidha, baada ya uchaguzi huo Mwenyekiti wa kamati hiyo aliyepitishwa Wise Mgina amewashukuru madiwani wote na kuwaomba kushirikiana naye katika masuala mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.

Amesema, nafasi hiyo ataitendea haki katika kuleta maendeleo, hivyo wakazi wa Ludewa wanapaswa kuwapa nafasi ya kufanya maendeleo viongozi wote waliopitishwa ndipo wawapime uwezo wao wa uongozi.

Ameongeza kuwa, kumekuwa na maneno mengi katika makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii yanayounganisha wakazi wa Ludewa yakijadili uchaguzi wa 2025 kitu ambacho si chema sana kwa kipindi hiki kwani viongozi walioteuliwa bado hawajaanza utendaji wao.

"Si vyema kuanza kuwajadili na kuwatolea kasoro viongozi waliopitishwa na kuanza kujadili uchaguzi ujao, tunaomba mtupe nafasi ya kuwaonyesha uwezo wetu kiutendaji ndipo mtujadili,"amesema Wise.

Naye Mbunge wa jimbo hilo, Joseph Kamonga amewaomba madiwani wote kuwa na ushirikiano ikiwemo kumshirikisha katika changamoto mbalimbali zinazowasilishwa kwao kutoka kwa wananchi ili kuweza kuzitatua na kuzijadili kwa pamoja.

"Mimi ni mbunge wa wote hivyo kila Diwani anapaswa kuwa huru kunishirikisha changamoto zilizopo ndani ya kata yake na kuzitafutia ufumbuzi,"amesema Kamonga.

Post a Comment

0 Comments