Tanzania imeitaka dunia na Jumuiya za Kimataifa kutambua kuwa kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuwahimiza Watanzania kusali na kuliombea Taifa kuondokana na maradhi ya COVID 19 kamwe haikuwa kauli ya kupuuza kanuni za kisayansi za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Akitoa
salam za Shukrani kwa Mungu na watanzania kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni hitimisho la
siku tatu za kumshukuru Mungu baada ya maambukizi ya virusi vya corona
vinavyosababisha ugonjwa homa kali ya mapafu COVID 19 kupungua nchini
katika Kanisa kuu la Mtakatifu Albano Dayososi ya Dar es salaam, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba
John Kabudi amesema licha ya kauli ya Rais kutaka watanzania kusali bado
serikali ilisisitiza kufuatwa kwa kanuni za kisayansi za kuepuka
maambukizi ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa,kunawa mikono na kuepuka
mikusanyiko isiyo ya lazima.
Ameongeza
kuwa hatua ya Tanzania kufunga maabara yake iliyokuwa ikipima virusi
vya Corona hapo awali kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kubaini kasoro katika maabara kuu,hatua hiyo iliifanya Tanzania kuchukua
hatua ya kujijengea uwezo wake wa ndani na kujenga maabara mpya yenye
uwezo wa kuwapima watu wanaodhaniwa kuwa na virusi vya corona maradufu.
Prof.
Kabudi amesema kupitia kwa waumini wa Kanisa kuu la Mtakatifu Albano
Dayososi ya Dar es salaam,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli anashukrani kubwa sana kwa Mwenyezi Mungu na kwa
Watanzania wote kwa kuitikia wito wake wa wananchi kuondokana na hofu na
badala yake wamlilie Mungu jambo ambalo maombi hayo yamejibiwa kwa
kupungua maambukizi licha ya uwepo wa ubashiri juu ya idadi ya
watakaoathirika na kufariki dunia kwa maradhi ya COVID 19 kufikia laki
moja kwa Tanzania pekee.
Akizungumza
wakati wa mahubiri Canon Francis Xavery kwa upande wake amemshukuru
Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kutofunga nyumba za
ibada ikiwemo makanisa na misikiti licha ya mashinikizo kutoka sehemu
mbalimbali jambo lilimfanya mwenyezi Mungu kusikia maombi ya watanzania
kwa kuwa walimwamini Mungu.
Padri
Jacob Kahemele wa Kanisa la Kuu la Mtakatifu Albano Dayosisi ya Dar Es
Salaam kwa upande wake amesema kanisa hilo limeungana na waamini nchini
kote kuitikia rai ya Mhe. Rais huku akiwataka watanzania kuacha kujipa
hofu hususani katika mambo ambayo yanapita upeo wa binadamu na badala
yake kila mmoja kwa imani yake kujinyeyekeza mbele ya Mungu ambaye ni
suluhisho la mambo yote yanayoonekana na yasiyoonekana.
0 Comments