WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115 na amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka asimamie mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
Vilevile,
Waziri Mkuu amemwagiza mkandarasi anayejenga mradi huo aukamilishe kwa
wakati kwa sababu imebainika kuwa mvua zinazoendelea kunyesha nchini
haziathiri utekelezaji wa ujenzi huo.
Waziri
Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi Mei 14, 2020) akiwa katika ziara
ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi huo. Amesema ameridhishwa
maedeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.
“Nimetembelea
eneo la mradi na kujionea shughuli zote zinazoendelea, kazi
inayofanyika ni ya uhakika huku kukiwa na matumaini makubwa ya
kukamilisha mradi mapema kabla ya muda uliopangwa.”
Mradi
wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji unajengwa na kampuni ya
Arab Construction kwa pamoja na kampuni ya Elsewedy Electric zote za
kutoka nchini Misri. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha Megawati 2,115
ambazo zitaingizwa kwenye grid ya Taifa na kuifanya nchi kuwa na umeme
mwingi na wa uhakika.
Mbali
na kuliwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika, pia mradi huo umewezesha
kupungua kwa changamoto ya ajira baada ya Watanzania wengi wakiwemo
wakandarasi kupata ajira za kudumu na za muda mfupi.
Kukamilika
kwa utekelezaji wa mradi huo, kutaiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi
kikubwa cha umeme kitakachosaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati
ikiwemo ujenzi wa uchumi wa viwanda na mradi wa reli ya kisasa.
Hafla
ya utiaji saini ya Mkataba wa Ujenzi wa Mradi ilifanyika jijini Dar es
Salaam, tarehe 12 Desemba, 2018 na kushuhudiwa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli na Waziri Mkuu wa Misri Dkt. Mostafa Madbouly. Mradi huu ni
njia sahihi ya kufikia Uchumi wa Viwanda ifikapo mwaka 2025.
0 Comments