NAIBU
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameutaka uongozi wa Kijiji cha
Buhunda maarufu kama Lushokela kilichocho wilayani Misungwi mkoani
Mwanza kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi wake ili kuwa na uelewa juu
ya masuala ya uwekezaji katika sekta ya madini.
Naibu
Waziri Nyongo alitoa maelekezo hayo Aprili 12, 2020 alipotembelea mradi
mpya wa uchimbaji wa madini unaomilikiwa na Kampuni ya Busolwa Mining
LTD uliopo katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, baada ya kuelezwa
ugumu wa mwananchi katika kupisha mradi kwa mwekezaji huyo na kudai naye
anataka kuchimba katika eneo hilo.
“Hapa
ni suala la uelewa tu, elimu ya uwekezaji katika sekta ya madini
inatakiwa kwa wananchi, na watoaji wa elimu wa kwanza ni ninyi viongozi
wa Serikali za vijiji na mitaa.
“Mchimbaji
akiomba na kupewa leseni mmiliki wa ardhi anapaswa kulipwa fidia na
kupisha eneo hilo ili kupisha shughuli za uchimbaji,”Nyongo alisisitiza.
Kufuatia
changamoto ya utoaji wa mizigo bandarini, Naibu Waziri Nyongo ameahidi
kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Taifa la Usafirishaji
(TASAC) kuhakikisha inaharakisha taratibu za utoaji wa mizigo bandarini
ili vifaa hivyo vitolewe kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
mikubwa ya maendeleo na kuwafanya wawekezaji kukamilisha miradi yao kama
walivyokusudia.
Kutokana
na changamoto ya ugonjwa wa Corona unaoikabili Dunia, uliopelekea
baadhi ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa ufungaji wa
mitambo mgodini hapo kutokupatikana kwa wakati, Naibu Waziri Nyongo
alisema, changamoto hiyo inaelekea ukingoni kwani nchi ya China ambako
ndiko vilikiagizwa vifaa hivyo tayari viwanda mbalimbali vimefunguliwa
na vinazalisha hivyo watarajie ukomo wa changamoto hiyo ndani ya muda
mfupi.
Kwa
upande wake Mkurugenzi na mwekezaji wa migodi ya Busolwa Mining, Baraka
Ezekiel alisema wameshakusanya mchanga wa dhahabu utakaoweza
kuchenjuliwa katika mgodi wao mpya wa Misungwi kwa muda wa mwaka mmoja
na kubainisha kuwa, kwa sasa wanasubiri kukamilika kwa ujenzi wa mradi
huo uliokwamishwa kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa janga la corona
duniani.
Akifafanua
suala hilo, Baraka alisema, baadhi ya vipuri vya kukamilisha ufungaji
wa mitambo katika mgodi huo ulisimama kutokana na uzalishaji wa vipuri,
hivyo nchini China kusimama, lakini pia wataalamu waliokuwa wakisaidia
ufungaji wa mitambo hiyo hawakuweza kurudi mara baada ya kusherehekea
sikukuu za mwaka mpya wa Kichina kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa
corona uliopelekea mipaka nchini humo kufugwa.
Pamoja
na hayo ameeleza changamoto nyingine kuwa ni pamoja na ucheleweshwaji
wa kutoa mizigo bandarini, umeme mdogo kwa ajili ya kuendeshea mitambo
yao, na mgogoro wa eneo baina yake na mwananchi anayedai kutaka kuchimba
madini katika eneo la leseni hiyo.
Akizungumzia
suala la ajira, Baraka alisema mgodi huo unatarajia kuajiri watumishi
wa kudumu wapatao 88 miongoni mwao saba watatoka nje ya nchi kwa ajili
ya kusaidia kuelekeza wazawa namna ya kuendesha mitambo hiyo na pia
itatoa ajira zisizo rasmi kwa watu 200 hivyo kufungua fursa za ajira kwa
watanzania.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameiomba Serikali
kufungua soko la madini wilayani humo na kubainisha kuwa tayari ofisi
yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini wamekwisha andaa jengo kwa
ajili ya soko hilo na kubainisha kuwa kinachokosekana ni mashine za
kupimia purity ya madini ya dhahabu sokoni hapo.
Sweda
alisema, kufunguliwa kwa soko hilo kutaisaidia Serikali katika suala
zima la ukusanyaji wa mapato, lakini pia kuwapa fursa wachimbaji wadogo
waliopo katika eneo hilo kuuza madini yao sokoni hapo kuliko kusafiri
mpaka Mwanza jambo ambalo linahatarisha usalama wao.
Akijibu
hoja hiyo ya Mkuu wa Wilaya Sweda, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha soko hilo linawezeshwa
mapema na kufunguliwa ili kuwezesha biashara ya madini wilayani hapo
kufanyika sokoni hapo.
0 Comments