Na. Angela Msimbira KAGERA
Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro Mkoani Kagera imeendelea kususua katika suala la ukusanyaji wa mapato na kusababisha maendeleo ya Halmashauri hiyo kuzorota kutokana na baadhi ya viongozi kushindwa kusimamia suala hilo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati akiongea na uongozi wa Mkoa wa Kagera kwenye ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Mkoani Kagera.
Mhe. Jafo amesema hali ya ukusanyaji wa mapato katika Mkoa wa Kagera ni nzuri isipokuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro ambayo hali ya ukusanyaji imekuwa ikisusua na kupelekea Halmashauri hiyo kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati.
“Halmashauri zinategemea makusanyo ya mapato kwa ajili ya kujiendesha, hivyo zikishindwa kukusanya mapato zinapelekea kushindwa kutimiza malengo waliojipangia kwa mwaka na kushindwa kutoa huduma bora kwa jamii.” Amesisitiza Mhe. Jafo
Anafafanua kuwa hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri hiyo hairidhishi kutokana na baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu kucheza na ukusanyaji wa mapato, hivyo kuisababishia halmashauri kuwa nyuma kimaendeleo.
Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Biharamuro kuhakikisha anasimamia suala la ukusanyaji wa mapato na kutoa adhabu kali kwa watumishi ambao hawafuati sheria, taratibu na miongozo kweye suala la ukusanyaji wa Mapato
Mhe. Jafo amewaagiza viongozi wote nchini waliopewa dhamana kuacha kufanyakazi kwa mazoea bali watumie taaluma zao katika kuwahudumia wananchi maskini wenye uhitaji katika jamii
Akikagua ujenzi wa Miundombinu ya barabara Mkoa wa Kagera Mhe. Jafo amesema ameridhishwa na ujenzi wa barabara hizo zilizojengwa chini ya mradi wa uimarishaji Miji (ULGSP) jambo ambalo limebadilisha sura na muonekano wa Mji huo.
Aidha Mhe. Jafo yupo kwenye ziara ya Kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Mikoa ya Rukwa, Mpanda, Kigoma, Kagera na Geita
0 Comments