TANGAZA NASI

header ads

Wanandoa watiwa Mbaroni kwa tuhuma za utapeli wa kutumia jina la Mama Janeth Magufuli

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. SOPHIA ELIA MWALUANDA [22] Mfanyabiashara na Mkazi wa Sistila Jijini Mbeya na 2. MPAJI SELEMAN MWINYIMVUA [38] Mkazi wa Manzese Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia akaunti feki ya “facebook” yenye jina la Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli Mke wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli.

Watuhumiwa wamekamatwa mnamo tarehe 28.04.2020 majira ya saa 15:00 Alasiri katika operesheni na msako uliofanywa huko eneo la Ikuti Sokoni, Kata ya Ikuti, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya.

Mbinu wanayoitumia watuhumiwa ni kufungua akaunti “facebook” yenye jina la JANETH MAGUFULI SACCOS na kuuaminisha umma kwa kuweka picha ya mama Janeth Magufuli na kisha kutangaza kutoa mikopo nafuu kwa sharti la muombaji kutuma kwanza fedha kiasi cha Shilingi 76,500/= kwenye namba ya simu waliyoiweka kama ada ya mkopo ili aweze kupata mkopo wa Shilingi Milioni 3,000,000/=.

Watuhumiwa wamekutwa na simu mbili aina ya Infinix Smartphone ambayo imetumika kufungulia akaunti hiyo ya “facebook” na simu aina ya Siccoo Mobile [Analogue] inayotumika kupokea fedha zinazotumwa na watu mbalimbali. Aidha watuhumiwa wamekutwa na fedha taslimu shilingi 470,000/= ambazo wamekiri kuzipata kwa njia ya udanganyifu kupitia akaunti hiyo feki.

Mtakumbuka Februari 21, 2020 huko katika Mji Mdogo wa Mbalizi Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliwakamata vijana kumi na moja [11] kwa tuhuma za kujihusisha na wizi kwa njia ya mtandao kwa kutumia akaunti feki za mitandao ya kijamii ikiwemo “facebook” wenye majina ya viongozi wa Serikali na Wasanii maarufu wa hapa nchini. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

WITO WA KAMANDA.

Natoa rai kwa watanzania kuheshimu ikulu kwani ni mahali patakatifu na hapachezewi kabisa, Chombo cha dola hakitavumilia kuona mtu wa aina yeyote kwa vyovyote vile akitumia jina la ikulu kuibia au kutapeli watu wengine.

Ninatoa wito kwa wananchi kuwa makini na taarifa mbalimbali zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaelekezea fursa mbalimbali kama vile ya mikopo, masomo na biashara ambazo zinawataka kutuma kiasi kadhaa cha fedha ikiwa ni moja ya masharti ya kupata fursa hiyo, ni vyema kujiridhisha kwenda mamlaka za serikali zilizo karibu kwa ajili ya kupata uhakika kabla ya kufikia uamuzi wa kutuma fedha.

Aidha ninawataka vijana kujenga utamaduni wa kufanya kazi ili kujipatia kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu ambavyo vitawasababisha kupata adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Mwisho, ninatoa rai kwa mtu/watu waliotuma fedha kupitia namba ya watuhumiwa kwa lengo la kupata mkopo kufika kituo cha Polisi kilichopo jirani kwa ajili ya kutoa taarifa ili taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.

Post a Comment

0 Comments