Na Mwandishi Maalum – Pwani
Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imejipanga kuwafikia walengwa wote waliostahili kupata chanjo na kuhakikisha kiwango kinabaki vilevile kama ilivyotarajiwa.
Hayo yamesemwa leo na Ofisa Mradi kutoka Mpango huo Lotalis Gadau wakati wa usimamizi elekezi wa kukagua utoaji huduma za chanjo katika Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na Engender Health kupitia Merck Sharp& Dohme B.V (MSD).
Gadau alisema kuwa katika kipindi hiki cha nchi kukabiliana na Ugonjwa wa Corona, Wizara imejipanga kuhakikisha watoa huduma wa afya wanaendelea kutoa huduma za chanjo kwa watoto wadogo pamoja na wasichana ambao walikua wapate chanjo ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi(HPV).
“Kama Wizara tumejipanga vizuri kwa kuhakikisha chanjo zote zinakuwepo kwa wakati kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha watoto wote waliokuwa wanatarajia kupata chanjo wanapata,na watoa huduma wanachukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huu”, Alisema walikuwa wakisikia wananchi wana wasiwasi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma,
"tumepita kwenye vituo vya afya kwenye mkoa huu na tumeona hali ni zuri kwani wazazi na mabinti wengi wanakuja kwenye vituo na tumewasisitiza kila mmoja anayeenda awe balozi anaporudi nyumbani kuhakikisha wataambiana ili kila anayestahili kupata chanjo anaenda kwenye kituo cha afya chochote cha jirani aweze kupata chanjo”.
Vile vile alisema kuhusu mabinti ambao walikua wapate chanjo ya kuzuia saratani ya malango wa kizazi tofauti na awali ambapo walikua wakifuatwa mashuleni ila kutokana na janga la Corona inasisitizwa wafike kwenye vituo cha kutolea huduma za afya vya karibu waweze kupata chanjo hiyo.
Upande wa watoto wadogo, Bi. Gadau amesema hivi sasa umewekwa utaratibu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili ambao wanastahili kupatiwa chanjo wao wanatakiwa kupata chanjo kama ilivyo kawaida
”Kwa kipindi hiki watoto ambao wamekamilisha ratiba ya chanjo na wanafika kituoni kwa ajili ya uzito tu wao wanatakiwa waende kila baada ya miezi mitatu hii ni kuepuka misongamano.
0 Comments