Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu Mhe. Stella
Ikupa amekabidhi msaada wa vifaa vya kukabiliana na ugonjwa wa
Corona kwa Shirikisho la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania
(SHIVYAWATA) kwa ajili ya kusaidia kundi hilo maalum katika kujikinga
dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona
(Covid-19).
Akizungumza
wakati akikabidhi vifaa hivyo ikiwemo ndoo za kunawia mikono na mashine
maalum ya kunawia pasipo kutumia koki “Free Hand Water Tape” Naibu
Waziri, Ikupa alieleza kuwa Serikali inatambua mchango wa Watu wenye
Ulemavu na ndio maana viongozi na wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza
katika kusaidia kwenye mapambano dhidi ya janga hili la Corona bila
kusahau namna ya kuwasaidia watu wenye ulemavu pia katika kuwawekea
mazingira wezeshi ya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Nikiwa kama mdau
nimeona umuhimu wa kukabidhi ndoo za kunaw
ia mikono 90 na mashine
maalum ya kunawia pasipo kutumia koki kwa ajili ya kusaidia watu wenye
Ulemavu katika mikoa 10 ikiwemo Dar es salaam, Dodoma, Kilimanjaro,
Arusha, Mwanza, Tanga, Pwani, Iringa na Morogoro,” alisema Ikupa
“Natambua kuwa
uhitaji wa vifaa hivyo pamoja na barakoa (Mask), Vitakasa Mikono na
Sabuni vinahitajika kwa wingi kwa ajili ya kusaidia watu wenye ulemavu
katika maeneo mengine, nitaendelea kuangalia suala la huu uhitaji ili
tuendelee kuwezesha kundi hilo maalum zaidi,” alisema
Aliongeza kuwa
Serikali imeandaa miongozo katika kipindi hiki inayotazamia namna watu
wenye ulemavu wanaweza kusaidiwa wakati huu ambapo mataifa mengi dunia
yanaangalia namna bora ya kukabiliana na ugojwa huo, akitolea mfano wa
vifaa vya kunawia ambavyo vimeboreshwa na kuwa jumuishi kwa watu wenye
ulemavu pia.
Aidha, Naibu
Waziri Ikupa alitoa wito kwa kundi hilo maalum kuendelea kufuata
maelekezo yanayotolewa na viongozi na wahudumu wa afya Pamoja na kujenga
tabia ya kusoma taarifa kwenye mitandao ya kijamii na meseji wanazopata
kupitia simu zao za mkononi juu ya kukabiliana na Ugonjwa wa Corona
(Covid-19).
Sambamba na hayo
Mheshimiwa Ikupa amewataka wadau mbalimbali wenye nia njema kuendelea
kujitokeza na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na
janga la ugonjwa wa Corona nchini.
Naye katibu wa
Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa
Dodoma Bw. Justus Ng`wantalima alitoa shukrani kwa Naibu Waziri na
Serikali kwa ujumla kwa kutambua watu wenye ulemavu na kuamua kutoa
msaada wa vifaa hivyo ambavyo ni rafiki kwa watu wenye ulemavu na
alieleza kuwa vitawafikia walemavu wengi nchini na watanufaika kwa
kujikinga na ugonjwa wa Corona.
“Haimanishi kama
mtu ni mlemavu basi hawezi kupata maambukizi ya ugonjwa huu wa corona,
ugonjwa huo unaweza kumpata mtu yoyote hivyo uwepo wa vifaa hivi
utasaidia watu wenye ulemavu kujikinga na janga hilo,” alieleza
Ng’wantalima.
0 Comments