Na Bilgither Nyoni,Makambako
Wanawake wanaonyonyesha wametakiwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya juu ya kujikinga na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona ili wasiweze kuambukizwa wao pamoja na watoto.
Hayo yamesemwa na mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe Dokta Alexander Mchome ambapo amesema endapo mama anaenyonyesha ataambukizwa virus hivyo atapaswa kuendelea kunyonyesha kwa uangalizi wa wataalam wa afya ili asimwambukize mtoto wake.
Aidha dokta Mchome amewataka wahudumu wa afya katika kila kituo cha kutolea huduma za kliniki za wajawazito na watoto ili kuhakikisha wanatoa elimu dhidi ya kujikinga na virus hivyo kila wanapoenda kupata huduma.
Hata hivyo amekanusha taarifa iliyokuwa inaenezwa kwamba katika halmashauri ya mji wa Makambako kuna mgonjwa wa corona na kusema kwamba taarifa hizo siyo za kweli hivyo wananchi wanapaswa kuzipuuza.
Nao baadhi ya wakazi wa makambako licha ya kukiri kuipata elimu hiyo lakini wameomba kuongezwa kwa watoa huduma kwenye vituo vya afya ili waweze kuwahudumia kwa haraka na kuepusha msongamano.
Hadi kufiki leo ripoti ya wizara ya afya imeripoti visa 94 vya wagonjwa wa CORONA huku 4 wakipoteza maisha na 11 wakipona.
0 Comments