Na Amiri kilagalila,Njombe
Chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe, kimefanikiwa
kumnasa na kumkabidhi kadi ya uanachama aliyekuwa diwani wa kata ya Mjimwema
mjini Njombe kupitia tiketi ya CHADEMA Abuu Mtamike huku kikikiri kuwa
amewasumbua kwa muda mrefu kama alivyowasumbua aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema
mkoa Fakii Lulandala.
Katika kikao cha kumpokea diwani huyo viongozi
mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi na serikali wamesema bwana Mtamike sasa
ameutambua ukweli juu ya kazi kubwa zinazotekelezwa na serikali chini ya Chama
tawala.
katibu wa CCM wilaya ya Njombe Hanafi Msabaha
anasema sasa viongozi wa CCM kata ya Mjimwema wataweza kumtumia Mtamike kwa
shughuli yoyote kwa kuwa hakuna ukakasi tena.
“Kama Mtamike alikuwa hafanyi vizuri nani angeweza
kukaa naye na kumrekebisha kwa wakati ule katika chama chake kisichofanya
vikao,hakuna kamati za siasa tofauti na Chama cha Mapinduzi,kwa hiyo kwa sasa mnaweza
kumfanya mtamike awe vile mnavyotaka”alisema Msabaha
Akizungumza mara baaa ya kukabidhiwa kadi ya CCM na
kula kiapo Abuu Mtamike amesema kilichompeleka Chadema mwaka 2010 sasa
kimepatiwa ufumbuzi na Rais Dokta John Pombe Magufuli.
“Tuliingia kama upinzani kwasababu tulikuwa tunataka
maendeleo lakini leo yale yote tuliyokuwa tunayataka Dkt,John Pombe Magufuli
ametenda”alisema Mtamike
Katibu wa vikao vya kamati ya maendeleo ya kata
ambavyo mwenyekiti wake alikuwa diwani Mtamike bwana Augustino Ngailo ambaye ni
afisa mtendaji kata ya Mjimwema amemtaka diwani huyo kuacha kuwa kigeugeu baada
ya kuingia CCM.
Katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoa wa Njombe Erasto
Ngole mbali ya kupongeza uamuzi wa bwana Mtamike kuhamia katika chama hicho
lakini ametoa onyo kali kwa wana CCM watakaobainika kujihusisha na vitendo vya
rushwa kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao pamoja na wanaotumia fedha zao
kuwanyanyasa wengine.
Mwezi Oktoba mwaka huu serikali ya Tanzania
inatarajia kuendesha zoezi la uchaguzi mkuu wa Rais,wabunge na madiwani
watakaoliongoza taifa kwa miaka mitano ijayo.
0 Comments