Na.Mwaandishi wetu,Chato
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
amewataka wataalam wa sekta ya mifugo kote nchini watumie muda mwingi
kwenda kuwahudumia wafugaji badala ya kukaa ofisini.
Prof.
Ole Gabriel ameyasema hayo mara baada ya kufika kukagua moja ya kliniki
za mifugo iliyopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita leo ambapo amemshauri
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Leonard Mwaisabula kutenga
kiasi cha fedha cha kuanza ukarabati wa kliniki hiyo na Wizara yake
itamuunga mkono kwa kukamilisha hatua zilizobaki.
"Ni
kweli Wizara ina mpango wa kukarabati kliniki zote za Mifugo hapa
nchini lakini kipaumbele chetu cha kwanza ni kwa zile halmashauri ambazo
zitakuwa zimeshaanza ukarabati kwa kutumia fedha za mapato yao ya ndani
hivyo kama Chato mkianza mapema Wizara pia itawapa kipaumbele na
hatimaye muwe mfano kwa wengine",Aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard
Mwaisabula amesema kuwa halmashauri yake itayafanyia kazi ushauri huo
kwa sababu wana shauku kubwa ya kuona kliniki hiyo inafanya kazi.
"Nimepokea
ushauri wako Mhe. Katibu Mkuu na kesho tutakutana kwa ajili ya
kuangalia mchanganuo wa fedha tulizokuwa tumetenga kwenye idara ya
mifugo ili kuona namna tunavyoweza kuanza na ukarabati wa kliniki hii
kwa sababu kwetu ina umuhimu Mkubwa sana" Alisema Bw. Mwaisabula.
Mara
baada ya kutoka kwenye eneo hilo Prof. Olr Gabriel alielekea kwenye
eneo la mnada wa Buzirayombo unapotarajiwa kujengwa mnada mkubwa wa
upili ambako alioneshwa kuridhishwa na usanifu wa michoro inayoonesha
namna mnada huo utakavyokuwa baada ya kukamilika kwake.
"Lakini
pia nimeona eneo hili la mnada litakuwa linajumuisha pande mbili
zinazotenganishwa na barabara hivyo Mkurugenzi kwa kushirikiana na
Wakala wa Majengo (TBA) ni lazima muangalie namna ya kufanya ili
kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wote wakiwa kwenye eneo la
mnada" Aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Pia
alipendekeza kutokana na michoro ya mnada huo kuonesha ni wa kisasa ni
lazima kuwe na mfumo mzuri wa matangazo ndani ya eneo la mnada, kituo
kizuri cha Polisi kitakachofanya kazi kwa saa 24, Mfumo wa kibenki na
huduma za afya zitakazowanufaisha wananchi wote watakaokuwa karibu na
eneo hilo la mnada, Runinga kubwa itakayoonesha kila kinachoendelea
Mnadani hapo na mfumo mzuri wa kuhifadhi idadi na aina ya bidhaa na
huduma zinazopatikana mnadani hapo ili kuwe na utaratibu wa kupata
taarifa zote muhimu ndani ya muda mfupi.
Kwa
upande wake Meneja wa TBA Mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jeffa
aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano Mkubwa
iliowaonesha mpaka sasa ambapo aliahidi kufanya kazi nzuri
itakayokamilika kwa wakati.
"Tunataka
kuhakikisha mpaka kufika mwisho wa Mwezi Mei tuwe tumekamilisha na
kuwasilisha hii hatua ya michoro yote ya mnada huu na tunataka kabla ya
kuvuka mwaka huu wa fedha mkandarasi awe site" Alisisitiza Mhandisi
Jeffa.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard
Mwaisabula alisema mradi huo kwao una manufaa makubwa kwa sababu
utaongeza kiasi cha makusanyo ya fedha za ndani na hivyo kuiwezesha
Halmashauri kuboresha miundombinu ya huduma mbalimbali za jamii kama
vile Elimu na afya.
credit:Fullshangweblog
0 Comments