Ofisi ya Waziri mkuu inaendelea na zoezi la kuratibu awamu ya pili
ya uendelezaji wa mji wa serikali eneo la Mtumba, makao makuu ya nchi jijini
Dodoma.
Awamu hii ya pili inahusisha Ubunifu na ujenzi wa majengo makubwa ya
Ofisi zitakazotumiwa na Wizara za serikali.
Akiongea, leo tarehe 20 Aprili, 2020, katika kikao cha
Kamati ya Makatibu wakuu na Wataalamu wa michoro ya Ubunifu na usanifu , Katibu
Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu, (Waziri Mkuu na Bunge), Tixon Nzunda, amefafanua
kuwa awamu hii ya pili ya mpango huo inajikita katika kuboresha ubunifu na
usanifu wa mji wa serikali, ulioko Mtumba, Jijini Dodoma.
Aidha,
kufanikiwa kwa mpango huo ni kutachangiza jiji la Dodoma kuwa jiji
bora na la kisasa linaloendana na mahitaji na mifumo ya majiji bora duniani.
Ili kufikia azma hiyo, tayari Timu ya Wataalam
imepitia michoro ya ubunifu na usanifu. Pia Wakala wa majengo Tanzania
(TBA), inaendelea kufanya kazi kwa karibu na Taasisi nyingine
zinazohusika na miundo mbinu katika mji wa Serikali kama vile TARURA, DOWASA,
TANESCO, ZIMAMOTO, TPDC, TTCL na EGA.
Hivi karibuni,Mwezi Februari mwaka huu,2020,Waziri Mkuu wa
Tanzania, Kassim Majaliwa
alizindua Mpango Kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo aliwataka
wadau mbalimbali kutoa ushirikiano kwa kiwango cha juu katika utekelezaji wa mpango
kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kulifanya kuwa jiji bora
na la kisasa nchini.
Serikali, kupitia ofisi ya waziri
mkuu inaendelea kutekeleza zoezi la kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Dodoma.
Tangu utekelezaji wa zoezi hilo uanze mwezi Septemba 2016.
Uamuzi wa
kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma ulifanyika mwaka 1973 ikiwa ni maelekezo
ya Chama cha TANU kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa
utawala wa awamu ya kwanza chini ya Uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere.
0 Comments