WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo ameagiza Shule zote za Sekondari nchini kutoka kwenye mfumo wa kufundishia kwenye maabara pekee na kuhamishia mafunzo ya vitendo nje ya maabara pia. Jafo ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea Shule ya Sekondari ya Mt Carolus iliyopo Manispaa ya Singida kujionea utafiti uliofanywa na wanafunzi wawili wa kidato cha kwanza kuhusu kilimo chenye kutumia maji kidogo kwenye umwagiliaji jambo ambalo amelisifu kuwa na kuwapongeza wanafunzi hao.
Amesema wanafunzi hao wakitoka nje ya maabara wataonyesha uwezo wao kwenye ubunifu walionao na kusaidia usafi wa Mazingira.
Amewataja wanafunzi hao waliobuni kilimo cha umwagiliaji kinachotumia maji machache kuwa ni Jordan Ombeni na Steven Tesha ambao ni wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Amebainisha kuwa kilimo hicho kinasaidia usafi wa Mazingira kwa sababu kinasaidia kuondoa plastiki zilizopo mitaani na hivyo kutunza mazingira.
" Hawa watoto wanahitaji pongezi kubwa sana, wamefanya jambo kubwa na hakika wanastahili kupongezwa na kusaidiwa zaidi ili kuweza kutunza hivi vipaji na uwezo walionao," Amesema Jafo.
Kwa upande wake mmoja wa wazazi wa wanafunzi wanaosoma hapo, Dk Ombeni Msuya amewashauri wazazi kusaidia kuendeleza vipaji vya watoto wao ili vije kuwa na manufaa makubwa kwao na Taifa kwa ujumla.
"Kama wazazi ni jukumu letu pia kuhakikisha tunalinda vipaji na uwezo wa Watoto, hili siyo jukumu la Walimu pekee ni wajibu wetu pia kuwawezesha watoto kutimiza ndoto zao ili kuweza kuja kutoa mchango wao katika Taifa lao," Amesema Dk Ombeni.
Nae mmoja wa wanafunzi waliofanya utafiti huo, Jordan Ombeni amemshukuru Waziri Jafo kwa kufika kujionea kazi waliyofanya akisema wao kama watoto imewapa motisha ya kufanya vizuri zaidi.
"Kwa kweli tunamshukuru Waziri Jafo kwa kufika kuona utafiti wetu imetupa hamasa ya kufanya vizuri zaidi, tunawashukuru Wazazi na Walimu wetu, malengo yetu ni kuja kufanya mambo makubwa yatakayosaidia Nchi yetu," Amesema Jordan.
0 Comments