Shahidi wa saba katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya na wenzake wawili, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha, Gwakisa Minga ameieleza mahakama kuwa Diwani wa CCM, Bakari Msangi alifika kituo cha polisi akiwa anavuja damu masikioni na kueleza kupigwa na Sabaya na wenzake walioharibu mfumo wa CCTV camera katika duka walilovamia.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo shahidi huyo alisema Msangi na wengine waliokutwa kwenye duka hilo pia walikuwa na majeraha ya kupigwa baada ya kutekwa, kuporwa na kuibiwa vitu.
Gwakisa alisema kamera nne zilizokuwa katika duka la Shaahidi Store ziligeuzwa na kuelekezewa ukutani ili zisirekodi matukio yaliyokuwa yanafanyika.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, shahidi huyo alisema Februari 12 mwaka huu saa 10 jioni aliongozana na Numan Jasin na Hajirin Saad kukagua duka hilo.
Mbele ya Hakimu Amworo, shahidi alisema walipoingia ndani walikuta vitu vikiwa vimevurugwa huku kukiwa na matone ya damu na majimaji.
Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa walipozichunguza kamera walibaini nne zilikuwa zimegeuziwa ukutani na mbili zikiachwa kama zilivyo ila hazijarekodi uelekeo wa matukio yaliyokuwa yakifanyika dukani humo.
Mbali na kubaini kamera hizo kuchezewa, katika meza ya kuhudumia wateja, Jasin alipokagua alidai mashine mbili za EFD zilikuwa hazipo, baadhi ya nyaraka na fedha hazikuwepo na akawaagiza wapelelezi alioambatana nao kuchukua maelezo.
0 Comments