TANGAZA NASI

header ads

WATU 204 WAFANYA UPIMAJI WA MAGONJWA YA MOYO BILA MALIPO KATIKA MAADHIMISHO SIKU YA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU DUNIANI

 


Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

18/05/2021 Watu  204 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo katika maadhimisho ya siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani yaliyofanyika jana katika viwanja vya ofisi ya Mkurugenzi wa manispaa ya Ubungo iliyopo Mbezi Luis eneo la Luguluni jijini Dar es Salaam.

Upimaji huo wa siku moja ulifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI)  kwa kushirikiana na wenzao wa manispaa ya Ubungo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samwel Rweyemamu alisema upimaji uliofanyika ni wa kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography-ECHO), umeme wa moyo (Electrocardiography-ECG), urefu, uzito, Shinikizo la Damu (PB) na kiwango cha sukari mwilini.

“Kati ya watu tuliowapima 30 hadi 40 walikuwa na shida ya shinikizo la juu la damu ambalo lilisababisha misuli yao ya moyo kutanuka na wote hawa hawakuwa wanajijua kama wanamatatizo mbalimbali katika mioyo yao”,.

“Wengine tuliowapima tuliwakuta wanashida kwenye Valvu, moyo kutanuka, umeme wa moyo, matundu kwenye moyo na mmoja alikuwa na shida ya mshipa mkubwa unaosambaza damu sehemu zote za mwili (Aorta) ulikuwa umevimba. Huyu tuliyemkuta na matundu kwenye moyo ni mtu mzima wa miaka 45”, alisema Dkt. Rweyemamu.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa manispaa ya Ubungo Dkt. Peter Nsanya aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kuona umuhimu wa kuadhimisha siku hiyo na kwenda kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo kwa wananchi wa manispaa ya Ubungo na vitongoji vyake.

Dkt. Nsanya alisema katika upimaji huo wananchi waliojitokeza kupima ni kutoka wilaya za Ubungo, Ilala, Kinondoni, Temeke  na Kigamboni na wengine walitoka mkoa wa Pwani na kulikuwa na huduma ya msaada wa kijamii kwa watu waliokuwa wanahitaji huduma hiyo.

“Kila mwananchi alipimwa wingi wa sukari mwilini, urefu na uzito na wengine ambao walionekana kuwa na dalili za ugonjwa wa moyo walifanyiwa vipimo zaidi. “Waliofanyiwa kipimo cha ECHO walikuwa 133, ECG 75, waliopewa dawa walikuwa 132 na 34 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa hivyo basi walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)”,.

“Kati ya watu 204 ambao tuliwafanyia upimaji ni 38 tu hawakukutwa na matatizo yoyote yale ya moyo hivyo basi ninawaomba wananchi wanaposikia mahali kunafanyika upimaji wa magonjwa yoyote yale wajitokeze kwa wingi kupima ili kujuwa kama wanamatatizo au la na kama wanamatatizo wataanza  matibabu mapema”, alisisitiza Dkt. Nsanya.

Naye Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji  alisema katika upimaji huo walitoa elimu ya lishe bora kwa wananchi na kuwaeleza umuhimu wa lishe katika afya zao wao binafsi na familia zao.

“Nilipata muda wa kutoa ushauri nasaha kwa  mtu mmoja mmoja wengi wa niliowaona  walikuwa na tatizo la uzito uliokithiri na hawakuwa wanatambua kuwa ni tatizo katika afya zao. Wengine walikuwa hawajijui kama wanashida  ya shinikizo la juu la damu na walikuwa wanatembea na kufanya shughuli zao kama kawaida”.

“Tulitoa elimu ya matumizi sahihi ya chumvi katika chakula na mlo kamili kwa mgonjwa wa shinikizo la damu, umuhimu wa lishe na uhusiano wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na lishe bora”, alisema Husna.

Alimalizia kwa kusema kuwa wanawake wengi walikuwa na shida ya uzito mkubwa ukilinganisha na wanaume hiyo ni kutokana na aina ya vyakula wanavyokula kabla na  baada ya kujifungua.

Nao wananchi waofika katika upimaji huo waliishukuru Serikali  kwa huduma hiyo na kuwaomba wataalamu hao wawe wanatoa huduma ya upimaji bila malipo mara kwa mara kwa kufanya hivyo kutawasaidia wananchi wasio na uwezo kiuchumi kupata huduma za matibabu ya kibingwa kirahisi zaidi.

“Mimi nilifika hapa kwa ajili ya kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo baada ya kupima nimekutwa na tatizo la moyo kutanuka. Nashukuru nimepewa dawa za kutumia za mwezi mmoja pia nimepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ninaenda kumjulisha mme wangu ili tujipange na kwenda kutibiwa huko”, alisema Halima Hussein mkazi wa Kibaha.

“Ninashukuru nimefanyiwa vipimo bila malipo yoyoye yale bahati mbaya nimekutwa na shida ya umeme wa moyo nimepewa dawa za kutumia pamoja na rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI pia wataalamu wameniambia  nisikate tamaa nitatibiwa na kupona maradhi haya”,alishukuru Joseph Mushi mkazi wa Kimara .

“Mimi nimefanyiwa vipimo sijakutwa na shida yoyote ile ya moyo, nashukuru nimepata elimu ambayo imenifanya kuelewa ni jinsi gani nitaweza kuutunza moyo wangu na kuepuka kupata  magonjwa haya hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi na kuepuka kula vyakula vyenye mafuta mengi na chumvi nyingi”, alisema Baraka Suleiman mkazi wa Temeke.

Katika upimaji huo kampuni za uagizaji na usambazaji wa dawa za binadamu za Phillips pharmaceuticals Ltd, Ajanta Pharma na  Astra Pharma (T)LTD zilitoa dawa bila malipo kwa wananchi waliokutwa na matatizo ya moyo, kisukari na kikohozi.

Post a Comment

0 Comments