TANGAZA NASI

header ads

Wakulima wa chai watakiwa kujengewa uwezo kwenye uzalishaji wa zao hilo

 


Na Amiri Kilagalila,Njombe


Wakulima wa zao la chai hapa nchini wametakiwa kujengewa uwezo juu uzalishaji wa zao hilo na kuongeza thamani ili liweze kupata masoko ndani na nje ya nchi.


Kauli hiyo imetolewa  na mratibu wa mradi wa Markup Tanzania Safari Fungo katika kikao cha  kuwajengea uwezo wadau wa chai nchini kilichofanyika hapa mkoani Njombe.


Amesema  wazalishaji wa zao la chai wanapaswa kupatiwa mbinu na kujengewa uwezo kuanzia wakati wa kuvuna, kuongeza thamani pamoja na namna ya kupata masoko ndani na nje ya nchi.


Amesema  ili wakulima na wazalishaji wafanikiwe wanapaswa kupatiwa mafunzo ya nadharia kwa kujengewa uwezo darasani na baadae shambani kuona namna mafunzo waliyoyapata wanavyoweza kuyabadili katika vitendo.



Amesema  mafunzo hayo yanaweza kufanikiwa na kuinua viwango vya ubora endapo wadau wa zao hilo wakiwemo viongozi kutoka serikalini na  wazalishaji wa zao hilo wadogo, wakati na wakubwa watashirikiana.


Amesema  hilo likifanyika zao hilo la chai kutoka Tanzania litaweza kupata masoko kuanzia ndani ya nchi na nje ya nchi hususani barani ulaya ambalo ndiyo wadhamini wa mradi huo.


"Ninaamini kupitia zoezi hili wakulima na wafanyabiashara watahakikisha mambo haya wanakwenda kuyatekeleza kwenye biashara zao" amesema  Safari.


Ofisa kutoka wizara ya kilimo makao makuu idara ya maendeleo ya mazao na masoko ya kilimo Fikiri Katiko amesema  kupitia mradi huo wa Markup kupitia ITC katika kuongeza thamani ya zao la chai ni moja ya kipaumbele cha serikali kwenye zao hilo.


Amesema  serikali imeweka maeneo muhimu manne katika kukuza na kuboresha mazao ya kimkakati ambayo ni pamoja na matumizi bora ya maji na ardhi, kuongeza uzalishaji na tija,  kuongeza thamani ya masoko.ya mazao na kuweka mazingira bora ya kufanya biashara.



Amesema  katika zao la chai kwa wastani uzalishaji ni tani elfu thelathini kwa mwaka ambapo asililimia thelathini ni wakulima wadogo na zilizosalia ni wakulima wakubwa.


"Katika chai kavu asilimia 85 inakwenda kuuzwa nje ya nchi na 15 inatumika ndani ya nchi kwenye viwanda vyetu kwa ajili ya kutengeneza majani ya chai" amesema  Fikiri.


Meneja mkuu wa kiwanda cha chai Ikanga Gerald Ngenzi amesema   sekta chai nchini inapitia wakati mgumu tofauti na miaka mitano iliyopita changamoto kubwa ikiwa kwenye suala la bei.


Amesema   zao la chai kama ilivyo kwa mazao mengine ni lazima liweze kushindana kimataifa lakini ili lifanikiwe katika ushindani huo lazima zao hilo liwe na ubora.


"Kupitia Markup wataalam mbalimbali wanafundishwa, kuwezeshwa ili kuhakikisha wanarudi shambani kutekeleza mafunzo waliyoyapata ili mkulima azalishe chai iliyo bora" amesema   Gerald.



Baadhi ya wakulima walioshiriki kikao hicho cha wadau wa chai akiwemo Kennedy Peter kutoka wilaya ya Tarime mkoani Mara amesema   kuanzishwa kwa soko la mnada wa chai hapa nchi utawawezesha wakulima kupata bei nzuri itakayosaidia kuboresha maisha yao.


Amesema   vile vile kupitia mnada huo utakaokuwa hapa nchini  taifa litanufaika kwa kupata fedha za kigeni ambazo zitasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.


"Vijana wengi hawajikiti katika zao hili kwasababu ya ugumu wake kwenye bei pamoja na masoko hivyo serikali inapaswa kuweka viwanda ili kuinua thamani ya zao .la chai" amesema  Kenedy.


Post a Comment

0 Comments