TANGAZA NASI

header ads

Serikali mbioni kuanzisha mnada wa chai Dar es Salaam

 


Na Amiri Kilagalila,Njombe


Serikali kupitia wizara ya kilimo kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine wapo katika mchakato wa kuanzisha mnada wa chai hapa nchini unaotarajia kuwepo jijini Dar es salaam.


Kauli hiyo imetolewa na ofisa kutoka wizara ya kilimo idara ya maendeleo ya mazao na masoko ya kilimo Fikiri Katiko kwenye kikao kilichokutanisha wadau mbalimbali  wa zao la chai hapa nchini kilichoandaliwa na kuratibiwa na mradi wa  Markup kilichofanyika hapa mkoani Njombe.


Alisema lengo la kuanzisha mnada huo ni kupunguza gharama za kusafirisha chai kutoka hapa nchini na kupeleka Kenya ambapo kwasasa mnada wa zao hilo.hufanyika.


Alisema endapo mnada utakuwepo hapa nchini utasaidia kupunguza gharama na pia kusaidia wakulima wa chai kupata bei nzuri ya kuuza zao hilo.


 Alisema kwa kuwa serikali inatarajia pia kutumia maabara ya hapa nchini  hivyo wataweza kuhakiki ubora wa zao hilo la chai itakayouzwa katika mnada huo tofauti na sasa ambapo maabara inayotumika ni ya huko nje ya nchi.



"Tumekuwa tukipeleka asilimia 80 ya chai yetu nje ya nchi lakini sehemu kubwa ya majani ya chai makavu huwa yanauzwa kupitia mnada wa Mombasa sasa serikali kwa kuona hilo lipo katika mchakato wa kuanzisha mnada wa chai nchini" Alisema Fikiri.


Mratibu wa mradi wa Markup Tanzania Safari Fungo lengo la kikao hicho cha wadau wa chai kusaidia wakulima na wafanyabiashara kuongeza thamani ya zao hilo na baadae waweze kupata masoko.


Alisema chai ni kinywaji cha pili ulimwenguni kinachonyweka zaidi baada ya maji hivyo ni lazima wazalishaji wa zao hilo wapatiwe mbinu na kujengewa uwezo kuanzia katika kuvuna, kuongeza thamani  hadi namna ya kupata masoko.



"Shughuli hii imegawanyika katika maeneo makuu mawili, kwanza sehemu ya nadharia ambapo wakulima na wafanyabiashara watapata nafasi ya kujengewa uwezo darasani na baada ya hapo tutaenda shambani wakaone namna yale mafunzo waliyoyapata wanaweza kubadilisha kwa vitendo" alisema Safari.


Meneja mkuu wa kiwanda cha chai Ikanga Gerald Ngenzi alisema sekta chai nchini inapitia wakati mgumu tofauti na miaka mitano iliyopita changamoto kubwa ikiwa kwenye suala la bei.


Alisema zao la chai kama ilivyo kwa mazao mengine ni lazima liweze kushindana kimataifa lakini ili lifanikiwe katika ushindani huo lazima zao hilo liwe na ubora.


"Kupitia Markup wataalam mbalimbali wanafundishwa, kuwezeshwa ili kuhakikisha wanarudi shambani kutekeleza mafunzo waliyoyapata ili mkulima azalishe chai iliyo bora" alisema Gerald.



Baadhi ya wakulima walioshiriki kikao hicho cha wadau wa chai akiwemo Kennedy Peter kutoka wilaya ya Tarime mkoani Mara alisema kuanzishwa kwa soko la mnada wa chai hapa nchi utawawezesha wakulima kupata bei nzuri itakayosaidia kuboresha maisha yao.


Alisema vile vile kupitia mnada huo utakaokuwa hapa nchini  taifa litanufaika kwa kupata fedha za kigeni ambazo zitasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.


"Vijana wengi hawajikiti katika zao hili kwasababu ya ugumu wake kwenye bei pamoja na masoko hivyo serikali inapaswa kuweka viwanda ili kuinua thamani ya zao.la chai" alisema Kenedy.

Post a Comment

0 Comments