Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema watoto wenye umri chini ya miaka 10 hawataruhusiwa kuhudhuria shughuli ya kutoa heshima za mwisho kwa Hayati John Magufuli kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na msongamano wa watu.
Akizungumzia na waandishi wa habari jijini Mwanza jana Mongella alitaja kundi jingine linaloshauriwa kufuatilia shughuli hiyo kupitia luninga badala ya kwenda uwanjani kuwa ni wenye maradhi mbalimbali pamoja na wazee.
“Maandalizi yote kwa ajili ya heshima za mwisho kwa Hayati John Magufuli katika viwanja vya CCM Kirumba yamekamilika. Hata hivyo, tunawasihi wazazi na walezi kuzuia watoto wadogo kuhudhuria shughuli hiyo kuepuka madhara ya msongamano. Wazee na wenye maradhi mbalimbali pia tunawashauri kufuatilia tukio hilo kupitia luninga,” amesema Mongella
Mkuu huyo wa mkoa amesema milango yote ya uwanja wa CCM Kirumba itakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi kwa ajili ya waombolezaji kuingia kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.
Kesho Jumatano Machi 24, 2021 wakazi wa Mwanza nao watapata fursa ya kumuaga kiongozi huyo atakayezikwa wilayani Chato Mkoa wa Geita Ijumaa Machi 26, 2021.
0 Comments