Na Paul Yohana Geita.
MAZISHI ya aliyekuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk.John Magufuli yamepangwa kufanyika kwenye makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwake wilayani Chato mkoani Geita.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea ratiba pamoja na hali ya maandalizi kuelekea kuupokea mwili wa Hayati Dk.Magufuli.
Mhandisi Gabriel alisema kwa muongozo uliopo ni kuwa utaratibu wa mazishi utasimamiwa na viongozi wa kitaifa, timu ya itifaki na wanafamilia ambao ndiyo pekee watahusika kumupumunzisha kiongozi huyo kwenye nyumba yake ya milele.
Alisema anafahamu kuna wananchi wengi ambao wana hamu ya kushiriki shughuli hiyo ya mazishi ya mpendwa wao siku ya tarehe 26 ambalo ni jambo jema lakini kutokana na muongozo uliopo haitowezekana kila mtu kushiriki.
"Kwa ujumla ni kwamba, kiongozi wetu atalazwa kwenye maeneo ya nyumbani, kwenye makaburi ya kifamilia, na eneo hilo lipo chini ya familia, utaratibu na maandalizi yanafanyika, tukio hili ni kubwa, niwasihi tu watakaopata kibari siku hiyo ya tarehe 25 na 26 ndiyo timu hiyo itashiriki pia nyumbani," alisema Mhandisi Gabriel.
Aidha mkuu wa mkoa ametoa wito kwa wananchi wote mkoani hapa kujitokeza kwa wingi maeneo ya barabarani siku ya tarehe 24 kumpokea na kumuaga Hayati Dk.John Magufuli ambapo mwili wake utawasili mkoani hapa kutokea mkoani Mwanza.
Alisema uongozi wa mkoa wa Geita umejipanga kuupokea mwili kuanzia mpakani mwa Geita na Mwanza ambapo msafara utakuja moja kwa moja na wananchi watakokuwa wameshajitokeza barabarani watakapewa fursa ya kuaga hivyo ni vyema wajiandae.


0 Comments