WAZIRI Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya, amemshauri Rais wa Sita wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuzingatia mambo matatu ya msingi ili kuongoza taifa kwa mafanikio.
Katika ushauri huo, Msuya ameyataja mambo hayo matatu kuwa ni pamoja na kuzingatia Ilani ya Uchaguzi, kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa pamoja na kujali changamoto za Watanzania wanyonge na hasa wanaoonewa.
Aidha, Waziri Mkuu Msaafu Msuya, amewatoa hofu Watanzania akisema ana matumaini makubwa nchi itapata maendeleo kwa kasi kama ilivyokuwa azma ya Rais John Magufuli ambaye amefariki dunia.
Msuya alisema hayo wakati wa mahojiano maalumu baada ya Samia kuapa kushika nafasi iliyoachwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Magufuli aliyefariki Machi 17, mwaka huu kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.
Alisema Rais Samia ameapa kuilinda na kuitetea katiba, hivyo miongozo ya msingi inapatikana katika kitabu hicho pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025 na si vinginevyo.
Alitaka umma kujikita kuyatazama, kuyatetea na kuyalinda maslahi ya taifa ili kuhakikisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ilani ya Uchaguzi ya CCM zinatekelezwa kikamilifu.
"Tanzania siyo nchi pekee duniani itakayoongozwa na mwanamke, Wajerumani wana Kansela, Angela Merkel, Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern na nchi nyingine nyingi tu; mbona zimepiga hatua za maendeleo? Mambo yatazidi kuwa mazuri, kila mmoja atimize wajibu wake kwa taifa," alisema.
Alisema Rais anapimwa kulingana na kazi anazofanya kwani awali alikuwa makamu wa rais wakati wa uongozi wa Magufuli, hivyo ana kila sababu za kufanya vyema katika utawala wake kutokana na ukweli kwamba mipango hiyo anaifahamu vyema.
"Hofu ya kutokujua aina ya rais anayekuja ilikuwepo hata wakati kabla ya kuapishwa kwa marais waliomtangulia Magufuli, lakini walipimwa kutokana na matendo yao hadi nchi imefika hatua hii ya maendeleo ya kujivunia; tungoje kazi ifanyike tusiwe na wasiwasi," alisema.
Msuya alisema kutokana na kupata fursa ya kuzunguka nchi wakati wa kuomba kura katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Magufuli na baadaye mwaka 2020 wakati wa kuomba ridhaa nyingine, Rais Samia anafahamu changamoto za Watanzania na namna ya kuzishughulikia kwa mafanikio.
Alisema ni wajibu sasa kwa Rais Samia kujielekeza katika miradi mikubwa ya kitaifa ikiwamo Bwawa la kuzalisha umeme la Mwl Julius Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), pamoja na changamoto zinazokabili Watanzania waishio mijini na vijijini.
0 Comments