TANGAZA NASI

header ads

Makonde ni mfano wa kuigwa,majengo ya kituo cha afya yavunja rekodi wilayani Ludewa

 


Na Amiri Kilagalila,Njombe


Wananchi wa kata ya Makonde wilayani Ludewa mkoani Njombe wameishukuru serikali kwa kuwaboreshea kituo cha afya na kuwa cha kisasa ambacho kipo katika hatua za mwisho za ujenzi wake kinachogharimu kiasi cha shilingi milioni 700 ambapo milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo matano na milioni 200 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba ambacho kinategemewa na wakazi zaidi ya 2500 wa kata hiyo pamoja na wananchi wengine kutoka kata za jirani.


Wametoa pongezi hizo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga wakati wa ziara yake katika kata za ukanda wa mwambao ambazo ni Lifuma, Lumbila, Kilondo,ikiwemo na kata hiyo ya Makonde akiwa ameambatana na kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa ukanda huo.

Ruben Masinka na Mariam Ngalawa ni miongoni mwa
wa wakazi wa kata hiyo wamesema kituo hicho kikikamilika kitakuwa na msaada kwao kwani kitawapunguzia kufanya safari kwenda katika hospitali ya wilaya kutibiwa ambapo hospitali hiyo ipo mbali huku wakikabiliwa na changamoto ya usafiri.


“Sasa hivi tayari tumepunguza ile kero ya kwenda wilayani na wagonjwa watatibiwa hapa bila ghalama kubwa ya kwenda Ludewa kwasababu mazingira yetu ni magumu sana na usafiri ni lazima uingie kwenye maji na wakati mwingine mgonjwa anaweza akafia hapa kutokana na dhoruba”alisema Ruben Masinka


Ashery Mwambalila ni afisa mtendaji wa kata ya Makonde,amesema utekelezaji wa kituo hicho cha afya umekamilika kutokana na nguvu kubwa ya wananchi kwa kushirikiana na serikali,aidha ameiomba serikali boti aina ya Ambulance ili kupunguza changamoto za usafiri kwa wagonjwa.


Naye diwani wa kata hiyo Crispin Mwkasungura amesema majengo hayo yakikamilika yatakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa tarafa nzima ya mwambao kwani kitakuwa kinatoa huduma za upasuaji hasa kwa wajawazito ambazo kwa sasa hazipatikani.


Amesema kwa sasa huduma hizo za upasuaji wanazifuata katika hospitali ya wilaya au wanalazimika kwenda matema mkoani Mbeya ili kupata huduma hizo kitu ambacho kinawafanya watumie gharama kubwa za usafiri na huduma nyinginezo.


Ameongeza kuwa pamoja na changamoto hizo za kituo hicho cha afya pia wanakabiliwa na uhaba wa walimu, miundombinu ya barabara, maji, uboreshaji uvuvi wa kisasa katika ukanda wote wa mwambao, umeme pamoja na huduma ya mawasiliano ya simu.


Aidha mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt,David Mwaka ameiomba serikali kuongezewa watumishi wa afya kwakuwa kituo hicho kina uhitaji wa watumishi 36 na kwa sasa kuna watumishi sita pekee mganga mmoja, muuguzi mmoja pamoja na wahudumu wanne na kupelekea kuwepo upungufu wa watumishi 30.


"Kutokana na uhaba huu wa watumishi inatulazimu kufanya kazi katika mazingira magumu kwani kituo cha afya kinapaswa kuwa wazi masaa 24 hivyo tumekuwa tukipeana zamu na watumishi wenzangu ili kuhudumu mchana na usiku ili wananchi wasikose huduima,hivyo tunaomba huu mradi uende na changamoto za kituo hasa upungufu mkubwa wa watumishi na nyumba za kuishi" Alisema Dkt Mwaka.



Kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amesema changamoto zote amezipokea na baadhi ya changamoto hizo tayari ameshaanza kuzifanyia kazi kwa kuzitafutia ufumbuzi.


Amesema kuhusu kuwepo kituo cha meli katika kata hiyo tayari ameshaanza kuwasilisha ombi hilo katika mamlaka husika na ataendelea kufuatilia mpaka atakapofanikisha suala hilo huku kuhusiana na watumishi amesema ataendelea kuikumbusha serikali kuleta watumishi hao katika sekta mbalimbali zenye mapungufu.


Pia amesema katika kukamilisha ujenzi wa vituo mbalimbali vya afya atakuwa sambamba nao katika kushirikiana kwani wananchi wamekuwa wakijitoa sana katika ujenzi huo hivyo jasho la wananchi halipaswi kupotea bure.


Sanjari na hayo pia mbunge huyo aliweza kutembelea shamba darasa la mihogo katika kata ya Lifuma ambalo limeandaliwa kwa mbegu alizowasaidia wananchi hao wa mwambao pamoja na tarafa ya masasi ambazo zina sifa ya kuzalisha kwa muda mfupi ukilinganisha na mbegu ambazo wanazitumia sasa ambazo wanavuna baada ya mwaka mmoja hadi miwili.

Post a Comment

0 Comments