Jeshi la polisi mkoani Njombe limesema mpaka sasa
wanashikiliwa watu wanne wakiwemo makada watatu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kwa tuhuma za mauaji ya Emmanuel Mlelwa mwanafunzi wa chuo
cha Tumaini Iringa ambaye ni mwenyekiti wa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu
(UVCCM) mkoa wa Iringa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa
akizungumza na vyombo vya habari,amesema jeshi hilo limewashikilia watu hao
kutokana na upelelezi wa awali wa mawasiliano yake.
“Jeshi la polisi lilianza upelelezi na tukajua mtu
wa mwisho aliyekuwa anaongea naye ni mtu mmoja anaitwa Tadei Mwanyika,huyu ni
mgombea udiwani kupitia kata ya Utalingolo,tulimkamata na hakuwa na maneno
mengi yeye anasema kweli nilikuwa na Marehemu”alisema kamanda Issa
Aidha amesema mtu wa pili kutambuliwa ni George
Sanga mgombea wa Udiwani kupitia Chadema kata ya Ramadhani ambaye gari yake
ilitumika kuwabeba watu hao akiwemo marehemu Emmanuel Mlelwa.
Vile vile amesema mtuhumiwa mwingine aliyeshikiliwa
ni Optatus Mkwera katibu mwenezi wa kata ya Ramadhani wa Chadema ambaye kwa mujibu wa maelezo yake ameeleza
tukio zima lilivyokuwa.
“Huyu naye alihusika kushiriki mauaji kwa mujibu wa
maelezo yake”alisema Kamanda
Mtuhumiwa wa nne ni Gudluck Mfuse anayejishughulisha na udalali wa
magari yanayobeba mbao na viazi ambapo kamanda wa polisi amesema tukio hilo
anaamini lilikuwa limepangwa na jeshi hilo linaendelea na upepelezi dhidi ya
mtandao huo ili haki itendeke.
Hata hivyo kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Hamis
Issa amesema gari namba T457 DAB Toyota Gaiya inayomilikiwa na George Sanga
mgombea wa udiwani kata ya Ramadhani ndio inayotuhumiwa kutumiwa wakati wa
utekelezaji wa mauaji ya Kada huyo wa CCM kutokana na kukutwa mkanda wa kiunoni
wa marehemu baada ya gari hiyo kushikiliwa.
Mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya
amesema mwili wa marehemu Emmanuel, ulikutwa eneo la bwawa la maji kibena na
alipotea tangu tarehe 20 mwezi wa 9 huku akiwa ni miongoni mwa vijana walioko
kwenye timu ya kampeni ya mgombea wa Ubunge jimbo la Njombe mjini.
“Kwa mara ya mwisho simu yake ilikuwa hewani tarehe
20 tangu hapo hakupatikana lakini kwa kuwashirikisha ndugu wa marehemu
ilibainika mwili uliokuwepo hospitali ni wa Emmanuel Mlelwa na ushahidi wa
awali unaonyesha ndugu Emmnuel ameuawa kikatili katika mazingira ya kisiasa”alisema
Marwa Rubirya
Hata hivyo uongozi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo Chadema kupitia kwa mwenyekiti wake Rose Mayemba wameliomba jeshi la
polisi kuweka wazi juu ya taarifa za wagombea wao bila kuharibu uchunguzi wao.
“Tunaliomba jeshi la polisi kama kuna mambo
inafuatilia ni vema sisi na wao kuwe na taarifa za wazi kama wamehusika na
mauaji watuambie lakini kitendo cha kuficha taarifa sahihi hatuwezi kuishi kwa
namna hiyo kwa kuwa wale ni wagombea”alisema Rose Mayemba
0 Comments