Na Amiri Kilagalila,Njombe
Serikali mkoani Njombe imetoa onyo kwa madereva wa boda boda, bajaji, daladala na taksi kuepuka kutumika vibaya na watu wenye malengo maovu hasa kipindiki hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani,wabunge na Rais.
Kauli hiyo imetolewa
na mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri akimuwakilisha mkuu wa mkoa wa Njombe
mhandisi Marwa Rubirya kwenye semina iliyoandaliwa ili kuyajengea uwezo makundi
hayo yaweze kufanya kazi kisasa pamoja na kuwaunganisha na fursa za kiuchumi
Vile vile amesema katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi umakini utakuwa wa hali ya juu kwani watu wa aina tofauti wataongezeka mkoani hapa tofauti na ilivyokuwa awali ambao wana tabia tofauti hivyo aliwataka wenyeji kukataa kutumika vibaya.
"Sisi wenyeji tuhakikishe kwamba Njombe tuliyonayo tunataka baada ya uchaguzi ibaki kama ilivyokuwa awali tukiwa na viongozi wapya watakaoenda kututumikia" Alisema Ruth Msafiri.
Aidha amesema makundi hayo yote ni wafanyakazi hivyo wanapokodishwa waendelee kufanya shughuli zao kwani wana vyombo vya usafiri ukizingatia kuwa kipindi hiki ni cha fursa hivyo wazitumie vizuri.
Aidha alizitaka
taasisi za fedha kuendelea kushirikiana na serikali na kukaa kwenye vikao vyao
ili kuona umuhimu wa kuhudumia vikundi hivyo kwa mtazamo tofauti na ule ukopaji
mwingine kwa kuangalia muda wa kudai marejesho pamoja na riba.
"Nchi yetu ina vijana wengi wa namna hivyo kwa kupata elimu hii itawasaidia kuanzia sasa na kuendelea kwa kufanya biashara zao kwa ufanisi" Alisema Mwang'onda.
Mratibu wa mafunzo ya usalama barabarani mkoa wa Njombe Koplo Marwa Kisyeli aliwataka waendesha vyombo vya moto kuzingatia elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na jeshi la polisi kaika kukabiliana na ajali za barabarani.
"Tumesema utaenda
mwendo kikomo maana yake ni mwendo ambao hutakiwi kuvuka lakini wapo madereva
taksi anaendesha gari spidi mia na bajaji pia chombo cha matairi matatu
kinatembea zaidi ya spidi sitini ikitokea ajali hapo ni kifo hivyo tutawaliwe
na elimu" Alisema Marwa.
"Boda boda wameonekana wakishiriki katika vitendo viovu lakini kupitia semina tuliyoipata tutabadilika na kufanya kazi zetu kwa uaminifu mkubwa" Alisema Alberto Myamba.
"Nimejifunza kama dereva unapokuwa unamiliki gari ni vizuri kukata bima kubwa ili hata chombo kikipata shida yeyote unaweza kulipwa" Alisema Yda Mlowe.
Mafunzo hayo
yalishirikisha madereva bodaboda, bajaji, dala dala, taksi, wadau wa
taasisi za fedha, bima ya afya, bima za mali pamoja na jeshi la polisi.
0 Comments