Baraza la Habari Tanzania (MCT), limesema kuwa waandishi waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbali mbali za kisiasa ni haki yao ya msingi kama walivyo raia wengine hapa nchini, lakini wanapaswa kuondoka katika uandishi wa habari.
Katibu Mtendaji wa MCT, Bw. Kajubi Mukajanga ameyasema hayo wakati wa mahojiano na waandishi wa habari katika ofisi za Baraza hilo leo (Julai 22, 2020), na kuongeza kwamba mwandishi wa habari kama sehemu ya jamii ana haki ya kuwa mpiga kura na pia ana haki ya kuwa mpigiwa kura.
“Hilo halina mjadala inatakiwa aondoke kwa sababu hakuna namna ambayo tutaendelea kumwamini wakati yeye amevaa shati la kijani, au la zambarau, au la blue na anapiga sera za chama, haiwezekani akaendelea kuwa ndani ya chumba cha habari,” alisisitiza.
Alisema waandishi wa habari wanapaswa kuliheshimu hili, lakini pia viongozi wa vyumba vya habari na wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kulisisitiza na kulitolea miongozo iliyo wazi ndani ya vyumba vya habari.
“Sisi tunavyoona ni kwamba, ikimpendeza mtu kwenda kwenye siasa, aende kwenye siasa moja kwa moja, akitaka baada ya hapo kujihusisha na kazi ya uandishi wa habari, ingependeza isiwe ndani ya chombo cha habari, kwa sababu watu wataendelea kumtazama kama mgombea, kama kada,” alisema Kajubi.
Alifafanua kuwa mwandishi wa habari ambaye amejihusisha na siasa za ushindani, anaweza kuwa mwana safu (Columnist) lakini chini ya safu yake ielezwe wazi kuwa huyu ni mwandishi wa siku nyingi na aliwahi kugombea kupitia chama flani cha siasa.
"Hii itasaidia hata mtu atakayeisoma safu yake au maoni yake aweze kujua mtu huyu anatokea wapi, na ana msimamo gani, hilo ni jambo la muhimu ambalo kila chombo cha habari ni lazima kikaweka utaratibu wake",alieleza.
Akizungumzia kuhusu chombo cha habari kuwa na msimamo na chama fulani, alisema si dhambi hata kidogo, na kuongeza kuwa katika historia ya vyombo vya habari hasa vya magazeti wakati yanaanzishwa huko Ulaya, yalikuwa yanaanzishwa yakiwa ya kutetea hoja za vyama vya siasa.
“Chombo cha habari kinaanzishwa na kinajulikana kwamba hiki ni cha mlengo wa kushoto, au cha sera za labour, hiki ni cha mlengo wa kulia, kinasimamia sera za conservative ndivyo vilivyoanzishwa,”alifafanua.
Aliwakumbusha waandishi wa habari kuwa kazi ya uandishi wa habari inamtaka mwandishi wa habari aonyeshe kwamba anaweza kutenda haki wakati wa uchaguzi kwa maana asipendelee upande wowote, wala asiuminye upande mwingine kwa faida ya upande unaoupenda yeye.
Aidha alivitaka vyombo vya habari vyenye lengo la kuonyesha mapenzi kwa chama fulani, kuweka wazi lakini nia hiyo, bali visigeuke kuwa vyombo vya propaganda kwa maana visiseme uongo, na badala yake viendelee kutoa haki sawa, visikandamize upande mmoja na visinyime upande mwingine haki ya kusikika, visiseme uongo, visipakazie upande mwingine kwa manufaa ya upande wake na visichanganye maoni ndani ya habari kwa manufaa ya chama chao.
Alisema waandishi wa habari wajitahidi kubaki kuwa wanahabari, “Mimi ningependa hii tasnia iwe na heshima, na iheshimiwe, ni kazi yenye majukumu makubwa, na ningependa waandishi wa habari wazuri wajitahidi kubaki katika taaluma hii,”alisema Bw. Kajubi.
Aliwaasa waandishi wa habari kutenganisha mapenzi ya kisiasa, ushabiki, na uandishi wa habari.
“Taaluma ibaki kuwa taaluma, na wanaotaka kwenda kwenye siasa, hawakatazwi waende kwenye siasa, na wafanye hivyo mapema, na wafanye hivyo kila mtu ajue, na wasiendelee kukaa ndani ya vyombo vya habari, au kukaa na vyeo vya kusimamia waandishi wa habari wakati wao tayari ni makada walioingia katika siasa za ushindani,” alisisitiza.
0 Comments