Na Henrick Idawa,Makete
Mahakama ya wilaya ya Makete mkoani
Njombe imemhukumu mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Iwale Mwl.Steven Mahenge
kulipa faini ya shilingi Laki 5 au kwenda jela miezi minne kwa kosa la kumpiga
na kumjeruhi mwanafunzi wake anayesoma darasa la 7 mwenye umri wa miaka 13
ambaye jina linahifadhiwa
Pia Mahakama hiyo imetoa amri ya
mshtakiwa kulipa fidia ya shilingi Laki 1 kwa mlalamikaji kutokana na kosa
alilomtendea lililopelekea kudhurika mwili wake
Hakimu mkazi wa mfawidhi wa mahakama
hiyo John Mpitanjia amesema shitaka hilo ni rufaa iliyokatwa na mlalamikaji
kutoka mahakama ya Mwanzo Matamba baada ya kuona kwamba hakuridhika na hukumu
iliyotolewa na mahakama hiyo ya mwanzo
Amesema katika shauri hilo baada ya
mahakama kupitia mwenendo wa kesi iliyosikilizwa na mahakama ya Mwanzo Matamba,
imebainika alishtakiwa chini ya kifungu ambacho hakikuwa sahihi kwa mujibu wa
kifungu cha 241 cha sheria ya kanuni ya adhabu 16 kama kilivyofanyiwa marejeo
2002, mshtakiwa akikutwa na hatia alitakiwa kupewa adhabu ya kifungo cha miaka
5 jela
Hakimu Mpitanjia amesema kwa mujibu wa
kifungu cha 21B cha Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, amebatilisha adhabu
iliyotolewa na mahakama ya mwanzo Matamba kumhukumu Mwalimu huyo kulipa faini
ya shilingi laki 1 ama kwenda jela miezi miwili pamoja na kumlipa mlalamikaji
fidia ya shilingi 87,000
Akijitetea mbele ya Mahakama hiyo kabla
ya hukumu kutolewa, Mshtakiwa huyo Mwl. Staven Mahenge amesema kwa kuwa ni kosa
lake la kwanza anaomba mahakama hiyo imsamehe na kumuachia huru kwa kuwa
anafamilia inayomtegemea, na wanafanya kazi kwenye mazingira magumu
Mpitanjia ametoa hukumu hiyo kwa
mshtakiwa na kusema rufaa iko wazi kwa upande wowote ambao haujaridhika na hukumu
hiyo aliyoitoa na wanatakiwa kukata rufaa ndani ya siku 30 kuanzia leo
Hata hivyo Baba Mzazi wa Mtoto huyo
Majaliwa Chawe nje ya mahakama amesema hajaridhika na hukumu hiyo huku akieleza
kukata rufaa upya kutoka na udogo wa adhabu hiyo huku yeye akiwa ametumia
ghalama kubwa kuanzia nauli na matibabu ya mgonjwa.
Mnamo Februari 18, 2020 majira ya saa
tatu asubuhi katika shule ya msingi Iwale wilayani Makete mkoani Njombe
mshtakiwa alimpiga kwa fimbo na mateke mwanafunzi wake (jina linahifadhiwa) na
kupelekea kumjeruhi kwa kumvunja mkono wake.


0 Comments