TANGAZA NASI

header ads

Bei ya ufuta yadorora, wakulima wauza kwa shingo upande


Na Ahmad Mmow, Lindi.

Bei ya ufuta kwa mnada wa tatu wa chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao imeshuka nakusababisha mvutano mkali baina ya wakulima waliokuwa wanataka usinunuliwe na wale waliotaka ununuliwe.

Katika mnada huo kwa msimu wa 2020 uliofanyika katika kijiji cha Kiranjeranje, wilaya ya Kilwa, bei ya juu ilikuwa shilingi 1,782 na ya chini shilingi 1,600 kwa kilo kilo moja. Huku ikishuhudiwa mvutano mkubwa baina ya wakulima ambao walikuwa wanakataa kuuza kwa bei hizo na waliokubali uuzwe. Hadi pale wakulima waliotaka uuzwe waliposhinda kwa hoja na kusababisha wenzao wakubali.

Juhudi kubwa iliyofanywa na kaimu mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika wa mkoa wa Lindi, Robert Nzunza akiungwa mkono na mmoja wa wakulima aliyekuwa kama msemaji wa wakulima waliotaka uuzwe, Mahadh Nangona zilisababisha wakulima ambao walikuwa wanaongozwa na Mohamed Maloi kutaka usiuzwe, wakubali kuuza ufuta huo wenye uzito kilo 4,693,913.

Awali wakulima hao walioongozwa na Maloi walisema bei hizo ni ndogo zikilinganishwa na gharama za uzalishaji. Kwahiyo ni bora usiuzwe na warudishiwe.

" Sasa kama Wachina wananunua kwa bei ndogo basi turudishiwe ili sisi wenyewe tupeleke kwa hao Wachina. Hatutaki, mnasema kinachosababisha ununuliwe kwa bei ya ndogo eti unachafu, ufuta safi huu uchafu upo wapi! wizi tu, tunaibiwa," walisikika baadhi ya wakulima wakisema.

Hata hivyo  Nsunza aliwaambia kushuka bei hakujaanza katika mnada huo bali hata maeneo mengine yanayolima ufuta, bei imeshuka.

Alisema bei ya ufuta haijaimarika sokoni. Kwani wanunuzi, hasa Wachina wananunua kwa shilingi 2,700 kwakila kilo moja baada ya ufuta kufikishwa bandarini ambako yanafanyika mauzo na manunuzi.

Nsunza aliwaeleza wakulima hao kwamba bei ya shilingi 2,700 imeendelea kusimama( kudumu) kwa muda mrefu. Huku ufuta ukiendelea kuongezeka.

" Kwamfano, wiki hii mkoani Mtwara bei ya juu ilikuwa shilingi 1,812 na Ruvuma ni shilingi 1,713. Kwahiyo hali hii siyo kwa Lindi Mwambao tu," alisema Nsunza.

Maelezo ya Nsunza yaliungwa mkono na mkulima Mahadh Nangona ambaye aliwasihi wakulima wenzake wakubali kuuza kwa bei hizo. Kwani hali hiyo inaashiria bei zinaweza kushuka zaidi. Kwahiyo watajilaumu na kuzikumbuka bei hizo.

" Tukumbuke yaliyotokea kwa wakulima wenzetu waliokataa kuuza korosho, hadi leo hazijanunuliwa.Pia sisi tunawawakilisha wakulima wote wa wilaya tatu, watu wanadhiki, wanataka fedha tutalaumiwa. Ufuta uuzwe," alisema Nangona.

Maelezo ya Nsunza na Nangona yaliwafanya wakulima wote wakubali kuuza baada ya kuulizwa na makamo mwenyekiti wa Lindi  Mwambao, Rashid Masoud ambaye alifanya kazi ya ziada kuwatuliza wakulima hao walioonesha kuwa na hasira kama walikubali kuuza au waliendelea kukataa.

Mbali na hayo, Nsunza aliwataka wanunuzi kulipa fedha za wakulima kwa wakati. Huku akiweka wazi kwamba minada kufanyika siku za Jumamosi na Jumapili nikuwapa nafasi wapate muda wa kuandaa malipo hayo.

Nsunza pia aliwaagiza watendaji na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika( AMCOS) wasisubiri wananunuzi waingize fedha kwenye akaunti ndipo waanze mchakato wa malipo. Bali  wanunuzi kabla ya kuingiza malipo waanze kuchakata malipo ili kuepuka ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima.

Bei hizo za leo nitofauti na bei za mnada wa pili uliofanyika katika kijiji cha Tulieni, manispaa ya Lindi. Kwani bei ya juu ilikuwa shilingi 2,115 na bei ya chini shilingi 2,046 kwa kila kilo moja.

Aidha kampuni zilizofanikiwa kununua ufuta huo ni SM Holdings, HS Impex Ltd, Hy sease,  RBST na Export Trading Ltd.

Post a Comment

0 Comments