Na Clief Mlelwa,Makambako
Wafanyabiashara mkoani Njombe wameshauriwa kutumia mitandao ya kijamii ikiwemo whatssap kuagiza bidhaa wanazozihitaji badala ya wao kusafiri ili kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu Unaosababishwa na virusi vya corona.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Njombe SIPHAEL MSIGALA huku akibainisha kuwa kwa hali iliyopo sasa ni vema wafanyabiashara wakatumia mitandao hiyo kuagiza bidhaa zao badala ya wao kusafiri.
Aidha mwenyekiti huyo MSIGALA amesema kuwa wafanyabiashara hawana haja ya kufunga biashara zao kwa kuhofia ugonjwa huo kwa kuwa endapo watafanya hivyo itapelekea adha kwa wananchi wa chini hasa wale ambao hawana uwezo wa kuweka akiba ya nafaka za chakula.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa makambako HANANA MFIKWA amewataka wafanyabiashara kukubaliana na kila hali ambayo wanakutana nayo kwa sasa kwa kuwa hata bidhaa ambazo walizoea kuzipata kwa wakati kwa sasa watachelewa kuzipata.
Nao baadhi ya wafanyabiashara mjini Makambako wamesema kuwa katika kukabiliana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona wamelazimika kutumia simu ili kupata bidhaa hizo japo kumekuwepo na changamoto ya kupata bidhaa ambazo hazina ubora.
0 Comments