TANGAZA NASI

header ads

Idara ya elimu Msingi na Sekondari Dodoma waanza kufundisha wanafunzi kupitia Radio



Na Jackline Kuwanda,Dodoma

Baada ya vyuo kufungwa pamoja na shule za msingi na sekondari kutokana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayo sababishwa na virusi vya corona (COVID-19) imeonekana kuwa baadhi ya wanafunzi walioko majumbani wamekuwa na muda mdogo wa  kujisomea tofauti na kipindi ambacho walikuwa Shuleni.

Kauli hiyo  imetolewa na Mtaalamu wa Elimu Mwalimu Dionisia Mbuva wakati akizungumza na maisha fm, ambapo amesema kuwa hiyo inatokana na baadhi ya wazazi  kushindwa kuwasimamia vyema watoto wao.

Aidha ,amesema kuwa kuna baadhi ya wazazi wamekuwa na uelewa wa kuweza kuwasimamia vyema watoto wao huku akigusia kwa upande wa wazazi ambao hata kipindi cha nyumba kabla ya ugonjwa huo hawakuwa na muda wa kuwafuatilia watoto na ameendelea kuwasisitiza wazazi katika kipindi hiki ambacho watoto wako majumbani kuwafuatilia kwa ukaribu kwani kuna baadhi ya watoto wamekuwa na tabia kukaa nje ya nyumba kwa nyakati za usiku huku wazazi wakiwa ndani .

Kituo hicho pia kimezungumza na mmoja wa wanafunzi anayefahamika kwa jina la Sharon Barnabas amesema kuwa kwa upande wake yeye anapata muda wa kutosha wa kujisomea kwa kufuata kile ambacho wameelekezwa na walimu wao.

Hata hivyo Idara ya elimu Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya jiji la Dodoma imeanza utaratibu wa kuwafundisha wanafunzi na kujikita zaidi katika madarasa ya mitihani kupitia Radio za Dodoma na mitandao ya kijamii katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona lengo likiwa ni kuwasaidia wanafunzi ambacho kwa sasa wako majumbani.

Ikumbukwe kuwa Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, aliwataka wanafunzi kuzingatia ratiba ya masomo inayotolewa ili wasikose vipindi huku  akilitaka pia Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA) na Taasisi ya elimu(TET)kuhakikisha utaratibu wa kufanya marejeo ulioanza kwa kidato cha sita uhusishe madarasa yote yanayotarajia kufanya mitihani ya Taifa.


Post a Comment

0 Comments