Kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Daniel Emmanuel (32) anashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukutwa na damu ya mama yake mzazi Eliyamulika Emmanuel Sarakikiya (79) kwenye kikombe.
Daniel ambaye ni mkazi wa Sakila wilayani Arumeru mkoani Arusha anadaiwa kumuua mama yake huyo kwa shoka na kisha kuinywa damu yake.
Akizungumza kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amesema mtuhumiwa huyo alifanya mauaji mnamo Mei 15 mwaka huu katika Kijiji cha Sakila chini, Kata ya Kikatiti, Tarafa ya King'ori wilayani Arumeru.
"Mtuhumiwa alimkata kwa shoka shingoni mama yake na kutenganisha na mwili wale na akaona haitoshi akakata mguu wa kulia na kuutenganisha na akakata mguu wa kushoto pia akautenganisha wakati anafanya unyama huu alikuwa anakinga damu kwenye kikombe anakunywa,"amesema Kamanda Shana.
Kamanda Shana amesema hata hivyo polisi walipofika eneo la tukio mtuhumiwa alitupa kikombe alichokuwa ameshika mkononi kikiwa kimetapaa damu na kujaribu kukimbia lakini alikamatwa na kuwekwa mahabusu kupisha uchunguzi.
Katika hatua za awali za uchunguzi inadaiwa mtuhumiwa huyo anamatatizo ya akili lakini Kamanda Shana ameonesha shaka juu ya hilo, ambapo amesema "lakini hili sikubaliani sana sababu aliwezaje kuandaa shoka, mazingira tulivu yasio na watu, pia kwanini kama hana akili alikimbia polisi alipowaona na alipokamatwa alikataa kuhojiwa na polisi, hili linanipa shaka".
0 Comments