Na Felix Mwagara, MOHA, Dar.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha
Mahabusu waliopo katika Magereza mbalimbali nchini wanaanza kufanya kazi kama
ilivyokuwa kwa wafungwa.
Amesema mchakato huo ambao tayari
umeanza, utakapo kamilika utaleta mapendekezo madhubuti ya jinsi gani ya
kuwatumia mahabusu hao pamoja na wafungwa katika kufanya kazi za uzalishaji
mali na kuhakikisha Jeshi hilo linajitegemea kikamilifu.
Akizungumza na Maafisa na Askari
Magereza katika Magereza ya Segerea, Ukonga na Keko jijini Dar es Salaam, leo,
kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya siku moja ya kusisitiza magereza
yanajitegemea nchini, alisema ili binadamu ale lazima afanye kazi, na pia
vitabu vitakatifu vinasisitiza hilo, hivyo mahabusu wanapaswa kufanya kazi kwa
kuwa nao wanakula vyakula magerezani.
“Kuna mjadala mkubwa tunaendelea
kuchakata kuhusu mahabusu waweze kufanya kazi, lakini lengo letu sio
kuwafanyisha kazi za sulubu, au kazi zinazotweza utu wao, hapana, wao pamoja na
wafungwa wana adhabu wanayoitumikia, tunataka kuwatumia katika kuzalisha,
kwahiyo watafanya kazi kama watu wengine wanavyofanya kazi, hili naomba
lieleweke,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “Mjadala
unaendelea na tutakuja na majibu jinsi ya kuwatumia mahabusu na wafungwa,
lakini tutakuja na majibu yenye mapendekezo tutashirikiana, lakini tunataka
kuwatumia kwa nia njema ya kuzalisha, kama mnavyojua binadamu asipofanya kazi
asile na imeandikwa katika vitabu vitakatifu, kama mtu umemfungia ndani alafu
hafanyi kazi na anadai chakula na ajue kwamba asipofanya kazi hana haki ya
kula, wewe umekuja ni mahabusu ili upeleke tonge hapa lazima uzalishe, huwezi
kusema sifanyi kazi kwasababu ni mahabusu, hapana tutakulinda hata kwa bunduki
utafanya kazi.”
Alisema lazima kuwepo na mtazamo
mpana, mkubwa katika masuala ya kuzalisha na kujitegemea kwa Jeshi la Magereza,
kwa ajili ya kuzalisha pamoja na kutatua matatizo mengine ndani ya Jeshi hilo
ikiwemo kujenga nyumba, kulipa umeme pamoja na mahaitaji mbalimbali ya Jeshi
hilo.
“Kama nilivyosema mjadala bado ni
mkubwa kwa wafungwa na tunafahamu wapo chini ya Magereza, lakini hao wengine
tumepewa tuwatunze wapo chini ya vyombo vingine, hivyo tunaendelea na mchakato
wa kujadiliana kuhusu hilo, na ukikamilika tutawaletea majibu,” alisema
Simbachawene.
Aliongeza kuwa, dhana ya Jeshi
hilo kuzalisha na kujitegemea ni agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt. John
Magufuli kulitaka jeshi hilo kuzalisha kwa wingi ili kujitosheleza na
kujitegemea.
Aidha, alilitaka Jeshi hilo
kuhakikisha Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam yaanze kufanya kilimo cha mboga
za majani na matunda pamoja na ubunifu wa uzalishaji mwingine katika mkoa huo,
na magereza yaliyopo mikoani yaendelee na kilimo cha mpunga, mahindi, ufugaji
pamoja na uzalishaji wa aina nyingine wanaoendelea nao katika maeneo yao.
Alisema kupitia uzalishaji mali
huo utawezesha kupata fedha baada ya kuuza na kusaidia majukumu mengine ya
Jeshi kuliko kutegemea fedha za matumizi mengine (OC) ambazo utolewa na
Serikali kwa Jeshi hilo.
Pia Waziri Simbachawene amelitaka
Jeshi hilo kuhakikisha wanahakiki mali zote za Jeshi ikiwemo mashamba yajulikane,
na pia ijulikane yana hati au hayana, na mifugo ya Jeshi hilo ipo wapi na idadi
yake ikiwa ni lengo la kutambua mali hizo na kuwekwa wazi kwasababu ni mali za
umma.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza
Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon Urio,
alimshukuru Waziri huyo kwa kufanya ziara katika Mkoa huo na kuwaomba viongozi
mbalimbali nchini waweze kutembelea magereza ili waweze kujifunza na kujua kazi
mbalimbali zinazofanywa na Jeshi mkoani humo.
“Tunakushukuru kwa kututembelea
Mheshimiwa Waziri, na maelekezo uliyotaoa tutayafanyia kazi, na pia tunawaomba
viongozi mbalimbali waweze kutembelea Magereza na kujua kazi mbalimbali
tunazozifanya,” alisema ACP Urio.
Simbachawene amemaliza ziara yake
ya siku moja kwa kutembelea magereza hayo, ambayo ni Gereza Kuu la Mahabusu
Segerea, Gereza Kuu la Ukonga na Gereza la Mahabusu la Keko, ambapo katika
ziara yake alipokua taarifa ya utendaji kazi kutoka kwa Wakuu wa Magereza hayo
pamoja na kuahidi changamoto zao kufanyiwa.


0 Comments