Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mpaluka Nyagali Mdude (32) ambaye
ni Kada wa CHADEMA Maarufu kwa jina la Mdude Chadema Mkazi wa Itezi
Jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na Unga unaodhaniwa ni dawa za
kulevya Aina ya Heroin. Akizungumza
na vyombo vya habari leo Jumatano May 13, 2020, Kamanda wa Jeshi la
Polisi Mkoa wa Mbeya Ulirich O. Matei amesema mtuhumiwa alikamatwa
May.10.2020 Jioni katika msako ulioyofanyika maeneo ya Kadege Stendi,
kata ya Forest, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya.
RPC
Matei amesema mara baada ya kukamatwa mtuhumiwa Polisi walikwenda
nyumbani kwake Mtaa wa Mwasote – Itezi Jijini Mbeya kwa ajili ya kufanya
upekuzi na katika upekuzi huo kulikutwa busta tano [05] za unga
udhaniwao kuwa dawa za kulevya aina ya Heroine wenye uzito wa gram 23.4
ambao ulikuwa umehifadhiwa kwenye mfuko wa kaki ambao ndani yake
kulikuwa na mifuko midogo miwili ya Nylon. Mtuhumiwa pia alikutwa na
simu mbili za mkononi aina ya Samsung na Nokia, CD 24 za aina
mbalimbali.
Amesema mnamo tarehe 12.05.2020 unga huo udhaniwao
kuwa dawa za kulevya ulipelekwa Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa uchunguzi zaidi wa kimaabara
na ilithibitika kuwa unga huo ni dawa za kulevya aina ya Heroine
Hydrochloride wenye uzito wa gram 23.4.
Aidha ameeleza kuwa,
Heroine Hydrochloride husababisha ulevi usioponyeka kirahisi [Drug
dependence] na hatimae husababisha mtumiaji kuharibikiwa na akili na
kwamba Dawa hizi pia zimo kwenye kundi la kwanza la orodha za sumu [Part
One Poison].
Amesema mtuhumiwa MPALUKA NYAGALI MDUDE pia alikuwa
anatafutwa kwa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi kwenye mitandao ya
kijamii dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania iliyopo
madarakani ya awamu ya tano.
Matei amesema Upelelezi wa shauri hili unaendelea, mtuhumiwa amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.
Kesi imeahirishwa hadi May 27,2020 na mtuhumiwa amerejeshwa mahabusu.
0 Comments