Uongozi wa Yanga umesema kuwa hauwezi kushindwa kuinasa saini ya nyota wa Simba, Clatous Chama iwapo watahitaji kumpata.

Kumekuwa na tetesi za Yanga kuiwinda saini ya Chama raia wa Zambia ambaye ana uwezo wa kubadili matokeo namna anavyotaka ambapo aliweza kufanya hivyo kwenye mechi mbili za kimataifa msimu wa 2018/19 mbele ya Nkana FC na AS Vita kwa kufunga mabao ya usiku.

Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema kuwa mpango mkubwa wa kuboresha kikosi chao upo na kutokana na uwepo wa kampuni ya GSM  hawashindwi kumpata mchezaji yoyote.

"Tunajua kwamba mashabiki wana shauku ya kuona kikosi bora na makini lengo letu ni kuwa na kikosi ambacho kitaleta ushindani hivyo ikiwa tutamhtaji huyo Chama haitakuwa kazi kumpata kwani kila kitu kinawezekana.

"Hatuna mpango wa kumfuata Zambia kwa sasa kwani mambo yamebadilika na mawasiliano yapo hivyo ni suala la kumalizana moja kwa moja ni suala la kusubiri," amesema.

Chama kwa sasa yupo Zambia ikiwa ni kwa ajili ya mapumziko ya kupisha maambukizi ya Virusi vya Corona.