Waziri
wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa amebainisha kwamba
Serikali imejipanga kuzalisha zaidi ya Barakoa Milioni tatu na nusu kwa
mwezi ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wote.
Hayo ameyasema
leo Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara ya Jijini Dar es Salaam ya
kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa (face mask) na Vitakasa mikono
(Hand sanitizer) ambapo kwa siku ya leo ziara hiyo imefanyika katika
Kiwanda cha Uzalishaji cha Prestine, Kiwanda cha Uchapishaji cha Five
stars na Kiwanda cha Uzalishaji Mafuta na Vilainishi cha Total.
Waziri
Bashungwa ameeleza kwamba Uzalishaji wa Barakoa za kutosha kwa sasa ni
muhimu sana na Serikali inahakikisha kwamba Viwanda hivi vinapata
malighafi ya kutosha ili viendelee kuzalisha vizuri.
“Kiwanda
cha Prestine sasa hivi kinatengeneza Barakoa elfu thelathini kwa siku
(30,000) lakini baada ya vifaa kuingia kitazalisha elfu hamsini kwa siku
(50,000) na Kiwanda cha Five Star kitazalisha barakoa laki moja kwa
siku (100,000) hivyo kwa ujumla Viwanda hivi vitazalisha barakoa
zisizopungua milioni tatu na nusu kwa mwezi mmoja (3,500,000) hii ni
hatua muhimu sana.”alisema Waziri Bashungwa.
Akizungumza
kuhusiana na ziara yake katika Kiwanda cha Total Waziri Bashungwa
ameeleza kwamba Uongozi umekubali kushirikiana na Serikali katika
kuzalisha vitakasa mikono na tayari maandalizi ya awali yamefanyika
ikiwa ni pamoja na kuangalia sehemu ambayo itatumika kwa ajili ya
uzalishaji.
“Baada ya kuangalia Kiwanda na eneo maalumu ambalo
wamelitenga kwa ajili ya uzalishaji wa vitakasa mikono, na kwa uwezo wa
kiwanda hiki kwa siku kitakua na uwezo wa kutengeneza lita elfu sita
(6000) ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kudhibiti ugonjwa huu.”
Aliongeza Waziri Bashungwa.
Katika hatua ya mwisho Waziri
Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuzingatia melekezo na
kanuni za kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona (COVID -19).
0 Comments