Umoja wa Ulaya, Urusi na Iran zimesifu maendeleo yaliofanyika katika mazungumzo juu ya mkataba wa nyuklia.
Mazungumzo hayo yalianza tena jana Jumamosi mjini Vienna kufuatia shambulio kwenye moja ya vinu vya nyuklia vya Iran.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya, Enrique Mora amesema maendeleo yamepatikana katika hali ambayo sio rahisi.
Naye balozi wa Urusi nchini Austria Mikhail Ulyanov amesema kuwa washiriki wa mazungumzo hayo wametambua na kuridhishwa na maendeleo yaliyopatikana na wameonyesha nia ya kuendelea na mazungumzo hayo.
Mazungumzo hayo yamefanyika siku moja tu baada ya Iran kutangaza kuwa imeanza kurutubisha madini yake ya Urani kwa asilimia 60 baada ya mlipuko katika kinu chake cha nyuklia cha Natanz, shambulio ambao Iran imedai limefanywa na Israel.
Msemaji wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki IAEA amesema shirika hilo, limethibitisha kuwa Iran imeanza mchakato wa kurutubisha madini yake. Iran imesema kiwango cha urutubishaji kilikuwa kimefika asilia 55.3.
0 Comments