Na Amiri Kilagalila,Njombe
Zaidi ya wazee 60 akiwemo mzee wa miaka 103 kutoka kijiji cha Itulike kata ya Ramadhani mjini Njombe,wamepokea msaada wa vitu mbali mbali ikiwemo sukari na sabuni kutoka mradi wa wazee ili kuwapunguzia ukali wa maisha.
Wazee hao kutoka kijiji cha Itulike pamoja na mtaa wa Kibena ambao wako chini ya mradi wa wazee unaotekelezwa na shirika la mwamvuli wa matumaini (Highland hope Umbrella) kwa kushirikiana na hospitali ya Tanwat,wameshukuru kwa kuendelea kuthaminiwa na kukabidhiwa misaada mbali mbali inayowawezesha kuendelea kuimarika kiafya.
Consolatha Mbata ni mzee mwenye umri wa takribani miaka 103 ameiomba jamii kuendelee kutoa msaada pamoja na kuwatunza wazee kama ambavyo wao wamekuwa wakipata msaada kupitia shirika hilo na kumuwezesha kuwa imara kimwili licha ya kuwa na matatizo ya macho pekee ambayo hayawezi kupona kwa sasa kutokana na umri wake kwa mujibu wa maelezo ya daktari wake.
“Ninaomba wengine wawe na tabia kama hii ya kuwaona na kuwatunza wazee,na mimi sasa hivi nguvu zimeisha na macho hayaoni na waganga wamesema macho yameharibika kabisa”alifafanua mtafsiri wa Bi Consolatha wakati wa mazungumzo.
Aidha licha ya kushukuru kwa msaada huo wa sukari,sabuni na nguo nzito (Mgololi) kwa ajili ya kujikinga na baridi amesema sababu za kufikia umri huo ni pamoja na kula vyakula vya asili huku akiendelea kumshukuru na kumuomba Mungu kumfikisha katika umri huo.
Atuendile Mgaya ni mwenyekiti wa kikundi cha wazee cha Asante chenye wazee 30 wa kijiji cha Itulike,kwa niaba ya wazee hao ameshukuru kwa misaada hiyo huku akiwashauri vijana kuwa na moyo wa kuwatunza wazee.
“Kwa kweli tunashukuru sana wametoka wanatulea mbali sana sio kwa leo tu,ninashauri vijana wafate mfano wa mama Liduke kwasababu anajitolea tu kwa ajili ya kutulea”alisema Atuendile Mgaya
Kwa upande wake Beth Liduke mkurugenzi wa shirika la mwamvuli wa matumaini (Highland hope Umbrella) wanao tekeleza mradi huo wa wazee amesema aemkuwa akikutana na wazee hao kila baada ya miezi miwili ili kuchunguza afya zao pamoja na kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao hali iliyopelekea tangu kuanza kwa mradi huo ni wazee watano pekee wamefariki dunia kati ya 65 na kubakiwa na wazee 60 katika mradi wao.
“Huwa tunakutana na wazee kila baada ya mizezi miwili,tunafanya mazoezi ya viungo,lakini pia tunaangalia afya zao na kuwakabidhi vitu mbali mbali ikiwemo sabuni na sukari kwa ajili ya kuwasaidia kupunguza ukali wa maisha.Hawa wazee afya zao zimeimarika na ninafurahi kwa kuwa afya zao zinazidi kuimarika na toka tulipoanza mradi huu tulikuwa na wazee 65 wamefariki 5 na tmebakiwa na wazee 60”alisema Beth Liduke
Edmund Mnubi ni afisa utawala wa hospitali ya Tanwat inayofanya kazi pamoja na shirika hilo katika mradi wa wazee.amesema kwa zaidi ya miaka 9 wamekuwa wakiwahudumia wazee hao huku wakikabiliana na maradhi mbali mbali ikiwemo magonjwa ya moyo,shinikizo la damu pamoja na matatizo ya mifupa yanayowakuta wazee mara kwa mara.
“Na tulivyoanza wengi BP zao zilikuwa juu sana lakini sasa hivi afya zao zinakwenda vizuri,wazee hawa tulipowakauta na sasa hivi kwa kweli ni tofauti na tunaamini huduma tunayowapa inawasaidia”alisema Edmund Mnubi
0 Comments